Ni matumizi ya lugha katika muktadha mbalimbali.Kuna sajili anuwai za matumizi ya lugha katika jamii. Hapa tutazingatia mifano michache ya sajili mbali mbali.Kila sajili huwa na sifa mbalimbali zinazoitofautisha sajili hiyo na nyinginezo. Ili kubaini sifa za lugha katika sajili fulani, ni muhimu kuzingatia baadhi ya maswali yafuatayo:
· ni mazungumzo baina ya nani na nani?
· kuna uhusiano gani baina ya wanaozungumza?
· yanapatikana wapi?
· yanatumika katika hali gani?
· yana umuhimu ama lengo gani
· ni istilahi zipi istilahi (maneno maalum) zinazopatikana katika mazingira hayo?
· umaizi wa lugha baina ya wazungumzaji ni wa kiwango gani?
· ni mtindo gani wa lugha unaotumika?
Sajili ya Ajali
Hii ni lugha inayotumiwa katika ambalo ajali imetokea. Wahusika wanaweza kuwa majeruhi, polisi, walioshuhudia au wananchi wengine n.k
Sifa za lugha inayopatikana katika sajili hii
1. Msamiati wa kipekee unaohusiana na ajali kama vile majeruhi, hudumanya kwanza, damu, mkasa.
2. Hutumia lugha ya kudadisi dadisi ili kubaini chanzo cha ajali.
3. Huwa na masimulizi – walio na habari kuhusu kisa hicho hueleza waliyoshuhudia
4. Kutokana na hali ya msukosuko, lugha hii haina utaratibu – watu huwa katika hali ya hofu, kwa juhudi za kuwaokoa majeruhi.
Mfano wa Sajili ya Ajali
Mwanakijiji 1:
Nimesikia twa! Kisha kishindo kikubwa sana (akihema hema) Nikaambia kuna mlipuko tukimbie.
Mwanakijiji 2:
Lilio la muhimu ni kuyaokoa maisha ya majeruhi kwa kuwapa huduma ya kwanza.
Mwanakijiji 1:
Tuondoeni miili ya waliofariki kwanza.
Mwanakijiji 2:
hatuwezi kuishika miili iliyobanwa katika gari hadi polisi wafike. Na ndio hao wanaokuja!
Mwanakijiji 1:
(akikimbia) Ndio hao! Acheni kuiba mafuta! Polisi wanakuja!
Polisi:
Wakitawanya wananchi walioliparamia gari kuiba bidhaa mbali mbali.Liinueni hili gari! Wapi dereva?
Dereva:
(ambaye amelala akihema kwa maumivu, damu ikichuruzika miguuni na mikononi) Nilisitishwa na ng'ombe waliokuwa wakivuka barabara. Nilijsribu kukwepa lakini usukani ukanishinda gari likapoteza mwelekeo…
Abiria:
Alikuwa akiendesha gari kwa kasi sana. Tukampigia kelele apunguze mwendo lakini hakutusikia. Matunda yake…
Mwanakijiji 2:
Niliona gari likibingiria mara kadhaa mpaka likaingia humu mtaroni, ndiyo tukakimbia kuwaokoa.
Polisi:
Nyamazeni! Achieni polisi kazi iliyobaki. Ikiwa kuna yeyote anayejuana na waathiriwa aandamane nasi.
Sajili ya Biashara
Lugha ya biashara huzungumzwa na wauzaji na wanunuzi katika sehemu za kibiashara. Inapaswa ikumbukwe kwamba lugha hii inaweza kubadilika kidogo kulingana na mazingira. Kwa mfano, katika mikutano ya kibiashara, lugha rasmi hutumiwa ilihali katika soko, lugha ya mitaani inaweza kutumika.
Sifa za Lugha ya Biashara
1. Hutumia msamiati wa kibiashara kama vile:
· Fedha
· Faida
· Hasara
· Bei
· Bidhaa
2. Hutumia misimu ili kuwavutia wanunuzi
3. Ni lugha yenye malumbano hasa watu wanapojadiliana kuhusu bei
4. Ni lugha legevu - haizingatii kanuni za lugha.
5. Huchanganya ndimi kwa kuingiza maneno ya lugha za kigeni
6. Ni yenye heshima na unyenyekevu kwa wanunuaji
7. Msamiati katika lugha ya Kibiashara
Mfano wa Sajili ya Biashara
Mtu X:
Tatu kwa mia! Tatu kwa mia! Leo ni bei ya hasara!
Mtu Y:
Unauza hii briefcase kwa pesa ngapi?
Mtu X:
Hiyo ni seventy bob mtu wangu
Mtu Y:
Huwezi kunipunguzia. Niuzie hamsini hivi.
Mtu X:
Haiwezekani mtu wangu. NItapata hasara nikiuza hivyo. Ongeza mkwaja, mama.
Mtu Y:
Basi hamsini na tano.
Mtu X:
Tafadhali ongeza kitu kidogo. Unataka nikule hasara leo? Fikisha sitini na tano.
Mtu Y:
Basi sitanunua hii. Sina pesa hizo zote. Unajua uchumi ni mbaya siku hizi.
Mtu X:
Tafadhali mtu wangu. Huu mkoba ni mzuri sana. Umetoka Germany. Angalia. Unaweka pesa hapa, kitambulisho hapa halafu unafunga hivi. Hauwezi kupoteza chochote ukiwa na mkoba huu. Angalia wewe mwenyewe. Hakuna mahali pengine utaweza kununua mkoba huu kwa bei ghali kama hii.
Mtu Y:
Nimekwambia sina hizo pesa. Nitanunua baadaye ukipunguza bei.
Mtu X:
Lete sixty bob. Lakini utakuwa umeniumiza. Nakufanyia hivyo kwa kuwa wewe ni customer poa.
Mtu Y:
Sawa basi nitanunua. Shika sixty bob.
Mtu X:
Asante Customer. Mungu akubariki. (akimfungia) Hey! Tatu kwa mia. Bei ya hasara! Tatu kwa mia!
Sajili ya Bungeni
Hii ni lugha inayozungumzwa wakati wa kikao cha bunge. Sajili hii ni tofauti na na sajili ya siasa, ambayo huhusisha wanasiasa wakipiga kampeni.
Sifa za Lugha ya Bungeni
1. Ni lugha yenye ushawishi – wabunge hutumia vishawishi ili kuwahimiza wenzao waunge ama kupinga msalaba
2. Ni lugha ya mjadala yenye waungao na wapingao.
3. Ni lugha yenye heshima na nidhamu. Maneno ya heshima kama mheshimiwa, tafadhali na samahani hutumika sana.
4. Hutumia maneno maalum yanayopatikana katika mazingira ya bunge kama vile kikao, mswaada, kuunga mkono, kujadili, kupitisha, n.k.
5. Lugha ya bungeni ni rasmi na sanifu.
6. Hulenga maswala mbalimbali ya kisiasa na maendeleo katika taifa.
7. Huwa na maelezo kamilifu
8. Ni lugha yenye maswali na majibu miongoni mwa wabunge.
Mfano wa sajili ya Bungeni
Spika:
Waheshimiwa, muda unayoyoma. Nawaomba mfanye mazungumzo yenu sauti ya chini tumsikize huyu. Endelea mheshimiwa.
Mbunge 1:
Asante Bwana spika. Hii siyo mara ya kwanza ya kuuwasilisha mswaada huu hapa. Kila mbunge anayethamini raia wa taifa hili ni lazima auunge mkono mswada huu. Katika kikao kilichotangulia, mliupinga mkidai kwamba hauna heshima kwa rais. Leo tumefanya ukarabati wote mliotaka. Hamna budi kuuunga mkono. Bwana spika….
Spika:
Muda wako umekwisha tafadhali keti. Wabunge wataamua hatima ya mswada huu ikiwa utapitishwa kama sheria. Lakini kumbukeni uamuzi wa mwisho ni wa rais
Sajili ya Hospitalini
Hii ni lugha ambayo huzungumzwa katika hospitali baina ya madaktari, wagonjwa, wauguzi n.k
Sifa za Lugha ya Hospitalini
1. Hutumia msamiati wa hospitalini kama vile
· dawa
· magonjwa
· Daktari
· Wadi
· Mgonjwa
· Dawa
· Kipimo
2. Ni lugha yenye upole na heshima
3. Huwa na maswali mengi hasa daktari anapotaka kutambua kiini cha ugonjwa unaomhadhiri mgonjwa wake
4. Ni lugha yenye hofu na huzuni
Mfano wa Sajili ya Hospitalini
Daktari:
Ulianza kuumwa hivi lini?
Mgonjwa:
Kichwa kilianza kuniuma jana jioni baada ya chajio. Nilipoamka asubuhi nikatambua kwamba hata tumbo lilikuwa likiuma pia.
Daktari:
Ulipoanza kuumwa na mwili mzima, ulichukua hatua gani? Hukunywa dawa yoyote?
Mgonjwa:
Nilichukua tembe zilizokuwa zimepatiwa kakangu miaka mitano iliyopita alipokuwa akiumwa na malaria.
Daktari:
Kila ugonjwa huitaji matibabu mbalimbali. Tembe za malaria haziwezi kutumika kutibu maumivu ya kichwa na tumbo. Pia ni hatari kutumia dawa ambazo zimepitwa na wakati. Zinaweza kukuletea madhara zaidi.
Mgonjwa:
(akikohoa) Sijui kama una tembe za kifua pia. Hii baridi inaniletea homa mbaya.
Daktari:
Hatuwezi kukupatia dawa kabla ya kutambua ugonjwa ulio nao. Itabidi tupime joto lako, damu na pia mate yako ili kupata tatizo linalokusumbua. Kisha tutakupatia dawa. Je, una umri wa miaka mingapi?
Mgonjwa:
Nikichukua hizo dawa nitapona?
Daktari:
Matokeo hubadilika kutoka kwa mgonjwa mmoja hadi mwengine. Inaweza kuchukua muda. Huenda ukalazwa kwenye wadi kwa siku mbili tatu hivi. Umri wako, mama?
Sajili ya Kidini
Katika sajili ya kidini tunaangazia lugha inayozungumzwa na waumini/washiriki wa imani fulani wakati wa ibada, sala, katika nyumba takatifu au mahali popote pale ambapo wanazungumzia mambo yanayorejelea imani au Mwenyezi Mungu.
Sifa za Lugha ya Kidini
1. Hutumia msamiati wa kidini kama vile
· Bibilia
· maombi
· mbinguni
· jehanamu
· Madhabahu
· Paradiso
· Mbinguni
· Mwenyezi Mungu
· Mwokozi
2. Ni lugha inayonukuu sana hasa wazungumzaji wanaporejelea Kitabu kitakatifu
3. Lugha yenye heshima, upole na unyenyekevu
4. Lugha sanifu
5. Ni lugha iliyojaa ahadi nyingi kwa wanaoandamana na mafunzo ya kidini na vitisho kwa wanaoenda kinyume na mafundisho
6. Huwa imejaa matumaini
7. Ni lugha yenye kutoa maneno ya sifa, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mfano wa Sajili ya Kidini
Boriti:
Bwana asifiwe Bi...
Bi Rangile:
Amina, mchungaji. Watoto wanaendeleaje?
Boriti:
Karita hana neno. Mwenyezi Mungu ametunyeshea rehema na neema zake. Je, wajukuu wako wa hali gani?
Bi Rangile:
Wanaendelea vizuri isipokuwa hawataendelea na masomo. Sijui nilimfanyia Mungu dhambi gani.
Boriti:
Nasikitika sana kusikia hivyo. Mungu atawalinda mayatima hao. Yeye ndiye baba wa mayatima. Mungu ni mwenye huruma.
Bi Rangile:
Sijui hayo, mchungaji. Hata sijui maana ya kuishi hapa duniani. Kila siku ni matatizo.
Boriti:
Usife moyo. Mungu anasema katika kitabu cha Yohana 14:18, "Sitawaacha nyinyi kama mayatima..." Kwa hivyo, ukiwa na imani, Mungu atakuonekania.
Bi Rangile:
Basi niombee mchungaji ili Saumu na Neema wapate karo ya kurudi shuleni.
Boriti:
Funga macho tusali. Ewe Rabuka uliyejaa neema na baraka tele. Tunakushukuru na kulitukuza Jina lako takatifu kwa baraka zako za ajabu. Tunajua kwamba wewe ndiye Mungu uliyewatoa wana wa Israeli kutoka Misri. Sisi wenye dhambi tunakuja mbele yako tukiomba ukafanya miujiza katika nyumba hii ya Bi Rangile......
Wote:
Amina.
Sajili ya Kisayansi
Sifa za Lugha katika sajili hii
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaoambatana na taaluma inayorejelewa.
2. Huwa na maelezo kwa ukamilifu.
3. Huwa na mpangilio maalum na maendelezo ya hoja na ujumbe.
4. Huchanganya ndimi na kutumia maneno ya kisayansi au lugha mbalimbali.
5. Hutumia lugha sanifu.
6. Ni lugha yenye udadisi mwingi (wakati wa kufanya utafiti)
Kwa sababu zisizoweza kuepukika, kikundi chetu hakitamaliza utafiti ulioratibiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi ujao. Hii ni kwa sababu ya changamoto kadhaa ambazo tumekutana nazo. Kwanza, viluwiluwi, ambao ndio tunaotafiti wamekuwa haba sana wakati huu wa ukame. Pili, kutokana na kufungwa kwa maabara ya kisayansi katika taasisi hii, ni muhali kufanya majaribio yoyote ya kazi yetu. Tatu, kumekuwa na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya wanakijiji kwamba kukusanya viluwiluwi kunawatia hofu. Aidha, tume yetu imepungukiwa na fedha baada ya serikali kusitisha kudhamini utafiti huu.
Baada ya kujadiliana kwa vikao tatu mfululizo, tume yetu inapendekeza haya: Muda wa kufanya utafiti uongezewe kwa kipindi cha miezi sita; serikali kupitia kwa taasisi hii ifadhili wachunguzi. Wananchi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa kuwafanyia viwavi utafiti na maabara ya utafiti ikaraatiwe haraka iwezekanayo.
Sajili ya Mahakamani
Hii ni lugha inayozungumzwa na wanasheria, mahakimu, mawakili, washitakiwa na mashahidi katika mahakama.
Sifa za Lugha ya Mahakamani
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaorejelea sheria kama vile
· katiba
· sheria
· mashtaka
· Hakimu
· Ushahidi
· Wakili
· Jela
· Mshitakiwa
· Kiongozi wa mashtakiwa
2. Huwa na maelezo marefu na ya kina ili kutafuta ushahidi wowote uliopo
3. Ni lugha yenye kunukuu sana hasa vipengele katika vitabu vya sheria kama vile katiba
4. Ni lugha rasmi na sanifu
5. Ni lugha iliyojaa maswali na majibizano
6. Ni lugha yenye heshima
Mfano wa Sajili ya Mahakamani
Kiongozi:
Musa Kasorogani, mwanaye Bi Safina na Mzee Mpotevu Kasorogani; umeshtakiwa kwa kosa la jaribio la mauaji mnamo tarehe 23/08 mwaka huu. Unaweza kukubali mashitaka, kukana au kunyamaza. Je, unakubali mashitaka.
Musa:
Naomba kukanusha mashtaka hayo, bwana mkubwa.
Kiongozi:
Je, kuna shahidi yeyote katika kesi hii?
Katili:
Hapa mkubwa. Siku hiyo ya tarehe 23/08, Musa alipatikana akiwa akijinyonga usiku wa maneno. Kijiji chote kilikusanyika hapo kwenye boma ya Kasorogani. Nilipoleta polisi, wakamkamata na kumpeleka hospitalini atibiwe kwanza. Ndiposa ameletwa hapa siku ya leo.
Kiongozi:
Je, mshitakiwa una tetesi lolote. Ama pia unaweza kuleta wakili wako azungumze kwa niaba yako.
Kisaka:
Bwana mkubwa, mimi ndiye wakili na shahidi wa Musa. Musa hakuua mtu. Alikuwa akijinyonga kutokana na mkasa uliomfika tarehe hiyo ya Agosti 23 baada ya bibi harusi wake kubadilika. Mimi na mamake, Bi Safina Kasorogani tulijaribu kumtuliza jioni hiyo. Asubuhi nilipoamka siku iliyofuatia, nikapata habari kwamba alikuwa amepelekwa hospitalini. Je, alipojaribu kujiua, alimwua mtu yeyote?
Kiongozi:
Kulingana na katiba ya nchi hii, kifungu cha 12.ab, kuua ni kutoa uhai wa binadamu yeyote. Haijalishi ikiwa ni yeye mwenyewe au ikiwa ni rafiki yake. Hivyo basi jaribio la kujiua ni hatia kulingana na kanuni za nchi hii. Una jingine la kuulizia?
Kisaka:
Je, sheria yetu inaruhusu mtu kuadhibiwa kwa kosa ambalo hakufanya?
Kiongozi:
La hasha.
Kisaka:
Basi tutakuwa tumekiuka kanuni za nchi yetu iwapo tutamhukumu Musa kwa kujiua ilhali hakujiua bado. Tunawezaje kutambua kama angekufa?
Katili:
Inafaa ahukumiwe kinyonga au kifungo cha maisha gerezani. Hata alivunja simu yangu...
Kiongozi:
Order! Lazima kutii mpangilio wa mahakama. Katili hauruhusiwi kuongea bila ruhusa ya hakimu au kiongozi wa mashitaka. Polisi, mpelekeni nje.
Sajili ya Matanga
Ni lugha inayotumiwa katika shughuli za mazishi au nyumbani kwa marehemu.
Sifa za Lugha ya Matanga/Mazishi
1. Hutumia msamiati wa maneno ya huzuni kama vile waombolezaji, makiwa, kifo, mauti, pole n.k.
2. Hutumia lugha ya kuliwaza/kufariji na kupa matumaini hasa kwa waombolezaji.
3. Ni lugha yenye unyenyekevu isiyotumia maneno yanayokera.
4. Hudhihirisha unyonge wa mwanadamu, kama asiye na mamlaka juu ya uhai wake.
5. Huwa na mbinu rejeshi kurejelea maisha ya marehemu alipokuwa hai.
6. Kwa mara nyingi hutumia maneno ya kusifu marehemu kutokana na aliyotenda.
7. Wakati mwingine huwa ni lugha inayodhihiri hali ya kukata tamaa.
Mfano wa Sajili ya Matangani
"Waombolezaji wenzangu, kama mnavyojua tumekusanyika hapa kwa ajili ya kumsindikiza rafiki yetu amabye amelala hapa. Ikiwa kuna mtu alifikwa zaidi na msiba huu ni mimi. Marehemu alikuwa rafiki wangu wa dhati tuliyeshirikiana naye sana. Nilimjua marehemu tukifanya kazi katika soko la Mauzoduni na tangu siku hiyo tumeishi kama ndugu; kuomba radhi ukikosewa; kusaidiana, na kadhalika.
Habari za kifo chake zilinipiga kwa mughdha. Sikuamini kwamba amekufa; kwamba sitamwona tena aushini mwangu. Ninasikitika sana lakini kwa kuwa Mungu hakosi, ninaamini kwamba alimpenda zaidi ya tulivyompenda. Ombi langu kwa Mungu ni moja, kwamba amweke rafiki yangu mahali pema peponi; au popote alipojitafutia siku zake za uhai; nami nitakapokufa anipeleke papo hapo tuendelee kuwa marafiki. Mwenzangu lala. Lala salama tutaonana siku moja"
Sajili ya Michezoni
Lugha ya michezoni hutumiwa wakati wa mashindano ya michezo kama vile kandanda, ukimbiaji n.k Hii inaweza kuwa lugha ya watangazaji/wasimulizi wa mchezo, watazamaji, mashabiki au wachezaji.
Sifa za Lugha ya Michezoni
1. Hutumia msamiati wa kipekee unaohusu michezo kama vile mpira, goli, mchezaji
2. Huchanganya ndimi na kuingiza maneno ya lugha nyingine kama vile Kiingereza. mfano 'goal!!!'
3. Ni lugha ambayo hutumia vihisishi na mshangao kwa wingi
4. Sentensi nyingi katika lugha hii huachwa bila kukamilika hasa hali inapobadilika uwanjani
5. Husimuliwa kwa haraka haraka ili kuambatana na kasi ya mchezo
6. Ni lugha yenye sifa na na chuku kwa mfano msimulizi anaposimulia sifa za mchezaji fulani
7. Hutumia misimu kama vile 'wametoka sare'
8. Hutumia kwa ya kulinganisha ili kuelezea matokeo ya mechi k.m 'walitoka mbili kwa nunge'
9. Ni lugha yenye kukariri (kurudia rudia) hasa mchezaji anapoumiliki mpira kwa muda mrefu au mwanariadha fulani anapoelekea kushinda katika mbio.
10. Huwa na sentensi fupi fupi
Mfano wa Sajili ya Michezoni
Nakwambia ndugu msikilizaji hapa mambo yamechacha kwelikweli. Hawa wachezaji wa Manyuu hawacheki na watu leo. Wameamua kuishambulia timu ya Cheusi bila huruma. Kumbuka kwamba hii ni mara yao ya... Lo! Anauchukua mpira pale, mchezaji nambari tisa... Matiksta. Matiksta, Matiksta na mpira. Anaucharazacharaza pale. Anamwangalia mwenzake. Anaupiga mpira kwa kichwa pale! Lo! Mwenzake anaukosa. Akiushika mpira pale ni mchezaji wa timu ya Cheusi, Romana. Romana, Romana anaelekeza mpira kwenye lango la Manyuu. Anaupiga mpira kwa nguvu! Lo! Hatari sana. Hatari sana katika lango la Manyuu. Hatari! hatari! Goooooooooo ooooh! Wameukosa! Goal keeper ameudaka mpira huo. Pole sana wachezaji wa ... Mlinda lango anaupiga mpira huo kwa hasira. Juu kabisa. Anauchukua pale nambari saba, Saruta. Huyu ni mchezaji machahari sana. Mwaka uliopita, alipewa tuzo la mchezaji bora wa mwaka. Ananyang'anywa na mchezaji mwingine hapa. Wanakabiliana kidogo. Huyu mchezaji anaupiga mpira kwa mguu wa kushoto. Lo! Mpira umekuwa mwingi na ukatoka nje.
Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...
Sajili ya Mitaani
Lugha ya mitaani ni lugha inayozungumzwa na vijana mtaani.
Sifa za Lugha ya Mtaani
1. Ni lugha legevu isiyozingatia kanuni za kisarufi
2. Huchanganya ndimi
3. Hutumia misimu kwa wingi
4. Hukosa mada maalum
Mfano wa Sajili ya Mtaani
Chali:
Hey, niaje msupaa?
Katosha:
Poa. So, mathee yako alikushow naweza kuja?
Chali:
Ha! Masa hana noma. Si unajua nita...
Katosha:
Chali! Unataka aniletee problem?
Chali:
Mimi ni boy wa maplans. Ngoja nifikirie venye tutamshow
Katosha:
Na by the way, kwani umejipaka mafuta ya manzi. Ama ulikuwa na msichana mgani?
Chali:
Oh! Niliscoop mafuta ya Anita. Si unajua nataka kunukia hmmmm...
Katosha:
Ok. So, umefikiria tumshow nini masa yako? Ama nikona idea poa.
Chali:
Nishow hiyo plot, na by the way, nataka unisaidie kuhusu ile deal yangu na Kaunda. Ile ya siz yangu.
Katosha:
Kwanza tutaplan na huyo siz yako, niwe ndiye nimekuja kuvisit. Mamako atakubali
Chali:
Wow! Idea poa. Utakuwa umekuja kufanya homework. Halafu masa akiishia kwa bed. Homework tutaitupa mbali.
Katosha:
So, utamshow Anita nakuja tufanye homework...
Sajili ya Nyumbani
Hii ni lugha inayotumiwa na watu katika familia. Wanaohusika sana katika mazungumzo ya nyumbani ni mama, baba, watoto, majirani na watu wa ukoo. Maswala yanayorejelewa sana ni yale yanayoiathiri jamii/boma hilo.
Sifa za Sajili ya Nyumbani
Sifa za sajili ya nyumbani hubadilika kulingana na mada inayorejelewa, wanaozungumza na hali katika boma.
Mfano wa sajili ya nyumbani
Baba:
Mama Kadara! Huyo mtoto wako amekuja?
Mama:
Kadara ni mtoto wetu; mimi na wewe.
Baba:
Hapana! Mimi sizai malaya. Huyo ni wako. Hata Bahati ni wako! Hakika wote sita ni wako…
Mama:
Mume wangu unanifanya nikasirike bure tu. Mbona umeanza mafarakano tena.
Baba:
Mafarakano! Mafarakano! Ni mimi niliyekwambia uzae wasichana sita…
Mama:
Lakini sikuzaa pekee. Tulizaa na wewe, mume wangu….
Baba:
Hapana! Uliniona na mimba? Uliniona na maumivu ya uzazi? Umeniona nikinyonyesha mtoto? Mwanamke kuwa na adabu. Nitakurudisha kwa wazazi wakufunze heshima. Na nitaoa sioni tukikaa pamoja.
Mama:
(baada ya kimya) Niambie ulichotaka kuniambia kuhusu Kadara (akijipangusa machozi kwa kitambaa) unajua mume wangu, nakuheshimu. Yangalikuwa mapenzi yangu tungepata wavulana pia. Lakini haya ni mapenzi ya Mungu.
Baba:
Kadara akija umpe kuku apeleke vileoni kwa Mzee Magoti. Nina deni lake kubwa baada ya kunywa tembo siku kadhaa bila kulipa. (akicheka) Hakika hata anastahili mbuzi.
Mama:
Hatuwezi kulipia pombe kwa mbuzi wala kuku. Kuku waliobaki hapa ni wangu na wa watoto wangu. Kuku wako uliwauza.
Baba:
Kelele za chura hazimkatazi ng'ombe kunywa maji. Endelea kupayuka kama wanawake wengine wa kijijini. Nikirudi nikute chakula na maji moto tayari.
Mama:
(akinuna) Haya nimesikia.
Sajili ya Shuleni
Hii ni rejista ya lugha inayopatikana katika mazingira ya shule. Wahusika wake huwa walimu, wazazi na wanafunzi.
Sifa za Sajili ya Shuleni
1. Matumizi ya istilahi (maneno maalum) yanayopatikana katika mazingira ya shule kama vile darasa, mitihani, vitabu, elimu, muhula, masomo
2. Lugha yenye heshima kutokana na utofauti baina ya mwanafunzi na mwalimu, mzazi na mwalimu;
3. Takriri - mbinu ya kurudiarudia maneno. Katika darasa mwalimu hurudia rudia maneno ili kusisitiza anachofunza
4. Ni lugha yenye maswali mengi na majibu. Mwalimu huuliza maswali wakati wa mafunzo. Wanafunzi pia huuliza maswali ili kujua/kupata ufafanuzi.
5. Hutumia lugha ya kukosoana na kurekebishana.
a) Mfano wa Mazungumzo katika Sajili ya Shuleni
Mwalimu:
Mzee Kundu, ningetaka tuzungumze kwa muda kuhusu hali ya mwanao, Machome Kundu.
Mzee:
Machome? Ana nini mwanangu.Kuna nafasi imepatikana ya…
Mwalimu:
Mwanako amebadilika sana kitabia. Alikuwa akifanya vizuri sana katika masomo
Mzee:
Kweli kabisa. Mimi ni mlezi mwema sizai watoto mbu mbu mbu darasani.
Mwalimu:
Ndivyo. Lakini sasa naona ameanza kubadilika. Ameanza kulegea katika mitihani na kuzembea kazini.
Mzee:
Unamaanisha nini? (akiinuka) Inaonekana siku hizi hamjui kuwapa adabu watoto. Ni lazima mtoto wangu amepotoshwa na wengine, katika vikundi vibaya!
Mwalimu:
Hakika, mwanako ndiye anayepotosha wanafunzi wengine. Yeye ni kiongozi wa makundi haramu shuleni, yanayovuruga masomo, kuuza dawa za kulevya na mambo kama haya. Hii ndiyo sababu nimekuita tujadiliane. Ni lazima mienendo hii imechipuka nyumbani.
Mzee:
Ajapo nyumbani, mwanangu huzingatia vitabu pekee hata mamake anaweza kuthibitisha haya. Ikiwa kuna utovu wa nidhamu nina hakika haya yanatoka darasani.
Mwalimu:
Tafadhali keti mzee (akichungulia dirishani) Mtindi! Niitie Machome…
b) Mfano wa Mazungumzo katika Sajili ya Darasani
Mwalimu:
Toeni vitabu vyenu vya Historia mnakili haya. Ni nani atakayetukumbusha tulichosoma wiki jana? Naam Halima!
Halima:
Tulisoma kuhusu Chama cha Mapinduzi
Wanafunzi:
(Wakiinua mikono na kupiga kelele) Mwalimu Mwalimu
Mwalimu:
Inueni mikono nitawaona. Msipige kelele. Halima umenoa. Simama! Mwanafunzi mwengine?
Jadaha:
Tulisoma kuhusu kundi asi la Maji Moto lililopinga wakoloni.
Wanafunzi:
Mwalimu! Mwalimu! Kundi la Maji Maji.
Mwalimu:
Naam mmepata. Lakini nimewaambia msijibu kwa pamoja. Ukitaka kujibu uinue mikono. Jadaha, ni kundi la Maji Maji siyo Maji Moto. Leo tutasoma athari za kundi katika taifa letu la Tanzania na namna lilivyoshindwa nguvu. Lakini kabla hatujaendelea ningependa mniambie, ni matatizo yepi yaliyochochea kuchipuka kwa kundi hilo.
Kirata:
Mwalimu nina swali. Kiongozi wa kundi hilo alikuwa nani?
Mwalimu:
Kirata hukuwa darasani wiki jana. Nione baada ya kipindi hiki. (wanafunzi wakicheka) Nawe wafanyani na kitabu cha Hisabati katika somo la Historia. Kimbia ofisini uniletee kiboko. Ninyi ndio mnaorejesha nyuma darasa langu katika mitihani.
Sajili ya Simu
Hii ni lugha inayotumiwa katika mazungumzo ya simu.
Sifa za lugha ya simu
1. Mazungumzo ya simu ni mafupi, hutumia sentensi fupi zenye muundo rahisi.
2. Hoja hutajwa moja kwa moja bila maneno mengi kwani ili kudhibiti gharama ya simu
3. Huwa na kukatizana kwa maneno kati ya wazugumzaji.
4. Huwa ni mazungumzo baina ya watu wawili pekee; anayepiga na anayepokea.
5. Hutumia istilahi maalum za lugha ya simu kama neno 'hello'
6. Huchanganya ndimi (kutumia maneno yasiyo ya lugha nyinginezo) ili kuwasilisha ujumbe kwa upesi.
7. Ni lugha ya kujibizana.
Mfano wa Sajili ya Simu
Sera:
Hello. Ningependa kuongea na Mika.
Sauti:
Subiri kidogo nimpatie simu.
Sera:
Hello
Mika:
Hello. Sema Sera. Niko kwa mkutano…
Sera:
Pole kwa kukusumbua. Unakumbuka safari yetu ya kesho?
Mika:
Siwezi kusahau. Tunakutana saa ngapi?
Sera:
nampendekeza saa tano machana…
Mika:
Katika Hoteli ya Katata Maa
Sera:
enhe. Hapo kwa heri
Mika:
Haya. Bye!
Maswali.
a)ainisha matawi ya isimu
1.Isimu saikolojia 2.Isimu falsafa 3.Isimu tumizi 4.Isimu tiba 5.Isimu Tiba 6.Isimu Fafanuzi 7.Isimu Jamii 8.Isimu Historia
b)ni nini maana ya fonolojia sintaksia mofolojia semantiki
Fonolojia ni tawi la sayansi ya isimu. Inashughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Matokeo ya uchunguzi wa kifonolojia yana umuhimu katika kubuni alfabeti. Dhana ya fonolojia inajipambanua vizuri zaidi ikifasiliwa kwa kutofautishwa na fonetiki. Wakati fonetiki ni taaluma inayochunguza sauti zitamkwazo na binadamu bila kuzihusisha na lugha yoyote, fonolojia huchunguza mfumo wa sauti wa lugha mahususi kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kimwera, na Kinyaturu. ZINGATIA: Fonetiki huchunguza sauti zote zitamkwazo na binadamu; fonolojia huchunguza MFUMO WA SAUTI wa lugha mahususi.
sintaksia ni aina ya sarufi inayojishughulisha na muundo wa maneno katika sentensi.pia hii tawi huhusika uchnganuzi wa aina za maneno,vipashio vya tungo pamoja na aina zake.
semantiki ni tawi la isimu linalojihusisha na uchunguzi na upambanuzi wa maana.ambapo maana inapambanuliwa na kupewa maana kamili au ya msingi. ingawa na maana za ziada huwepo. mfano, neno mama. maana yake ya msingi kabisa ni mzazi wa kike. wakati maana za ziada ni kama vile mtu yeyote ambaye ni mlezi wa familia,pia kama mke wa mtu.
MASWALI
.
a)Fafanua dhana hizi(alama 3)
i)Lafudhi
ii)Krioli
iii)Lahaja
b)Hujambo: You look familiar Nilikuona wapi my friend?
i)Mtindo huu wa kutumia lugha unaitwaje? Eleza (alama 2)
ii)Eleza sababu tatu kutumia mtindo huu wa lugha(alama 3)
iii)Pendekeza njia tatu za kuondoa mtindo huu wa lugha(alama 3)
c) Taja na ueleze sifa tano za lugha ya michezoni (alama 10)
educative with alot of information,,thank you very much.blessings be unto you
ReplyDeleteReally helping blog.. Thanx@ukumbi
ReplyDelete