Sunday, 29 January 2017

Uchambuzi wa kifo kisimani

TAMTHILIA YA KIFO KISIMANI 

UTANGULIZI 
Tamthilia ya Kifo Kisimani imeandikwa na kithaka wa Mberia. Toleo la kwanza la kitabu hiki ililikuwa mwaka wa 2001 na kina chapa nyingi hadi kufikia mwaka wa 2009.kimechapishwa na Marimba Publications Ltd. Anwani Anwani huwa ni jina la kitabu.Mwandishi amefaulu kutumia anwani’Kifo Kisimani’. Anwani hii inaashiria kifo cha Mwelusi pale kisimani alipouliwa na Gege. Pia anwani hii inaashiria kifo cha Wanabutangi baada ya kukosa maji pale kisimani.Hii ni baada ya kanuni mpya za utekaji maji kutolewa amabazo ziliwanyima haki za kuteka maji. Maji ni uhai hivyo kupewa siku tatu za kuteka maji ni kunyimwa uhai yaani kifo. Jalada Jalada ni karatasi ngumu inayofunika kitabu ambapo jina la kitabu huandikwa.Katika tamthilia hii kuna picha ya mtu aliye na huzuni.Mtu huyu ni kama ako katika shimo. Hii inaashiria shimo la mateso ambalo Wanabutangi wametiwa na utawala mbaya wa Bokono na vibaraka wake. Kuna picha inayoashiria machea.Hii inaonyesha matumaini kwa Wanabutangi baada ya Mwelusi na wenzake kuanza harakati za mabadiliko.Rangi inayotumika kwa picha ni ya udongo, kuashiria rotuba ya Butangi. DHAMIRA YA MWANDISHI Kiini cha jambo au habari iliyoandikwa na mwandishi.Katika Kifo Kisimani Kithaka wa Mberia ananuia kuamsha au kumchangamsha msomaji kuhusu utawala mbaya na jinsi ya kuleta mabadiliko na kuuondoa . Mwandishi anatetea haki za walionyanyaswa.Hivyo lengo kuu la mwandishi ni kuzindua watu. PLOTI Huwa ni mtiririko wa matukio katika kitabu.Tamthilia hii ina onyesho kumi.Muhtasari wa onyesho hizi ni kama ifuatavyo. Onyesho la kwanza Mchezo unaanza asubuhi ambapo viti vimepangwa tayari kwa mkutano wa Bokono.Mwelusi ambaye ni kijan anaingia uwanjani.Mawazo yake yanadhihirika kupitia kwa sauti tunayosikia .Yanamkejeli Bokono kwa ubinafsi wake na kuwanyanyasa wanabutangi. Kaloo anaingia uwanjani kwa kutayarisha ,anamwona Mwelusi na anadhani ni mmoja wa waliohudhuria lakini Mwelusi anamwambia alikuwa anapita tu ni mawazo yaliyomshika mguu.Kaloo anafurahi kwa kuwa Mwelusi anawaza juu ya Butangi si kama vijana wengine wanavyo waza kuhusu anasa. Mwelusi anakubaliana naye na kuongeza kuwa ni wakati wa vita. Kaloo hakubaliani naye na anamuomba amfafanulie matamshi yake. Mwelusi anamwambia kuwa atamueleza siku nyingine kwa kuwa hahudhurii mkutano na anaondoka. Mwelusi Batu anaingia kuukagua uwanja, anafurahishwa na viti.Anapoelezwa kuwa Mbutwe seremala aliyeunda viti anadai kulipwa Batu anasema aje amwone na amdai malipo ya mbuzi wawili. Wanawake ndio watakaocheza katika mkutanowa Bokono Mtemi wa Butangi.Batu anasema kuwa mtemi akifurahi,wanawake watafurahi.Azena anaingia uwanjani ili kumsaidia kaloo kwa matayarisho. Batu anaapoondoka Atega anaingia akifuatwa na Mwelusi. Wanashukiwa kuwa wapenzi kwa kuwa kila mara wanaonekana pamoja.Naye kama Mwelusi, anawafahamisha hatohudhuria mkutano.Batu anaingia tena uwanjani na kuamrisha watu waitwe.Gege anaingia uwanjani huku akiwa anapuliza ala ya muziki. Batu anamwambia ni muziki wa kuvutia, yeye anasema kuwa anausifia uongozi wa busara wa Butangi. Kaloo anamhakikishai kuwa yeye na jamaa zake ni wazalendo kamili na hawatasita kuhudhuria mkutano. Batu anawasaidia kujitayarisha jinsi watamsifia Bokono;Bokono Bokono milele!! Baada ya muda kidogo wanagundua kuwa watu hawaji kwa mkutano.Kaloo anaenda Mingamiwili na kurudi lakini hakuwapata watu huko pia. Bokono anapofika anapata hakuna watu kwa uwanja anakasirika sana. Vibaraka wake wanamuahidi kuwa kuna tatizo lakini watalinyoosha. Zigu anasema kuwa watu wamechochewa na Mwelusi.Hata hivyo Batu anasema kuwa watamkomesha anayewachochea watu.Baada ya mabo kutulia wote wanaanza kumsifia Bokono ;Utaongoza Butangi kwa miaka mia moja. Onyesho la pili Matukio ni katika makazi ya Mtemi Bokono amabayo ni sehemu ya majengo ya Utawala wa Butangi.Bokono amesimama huku akiangalia vitu vilivyo ukutani na mara kwa mara anaguza hiki na kile.mkewe Nyalwe amekaa kitini raha mustarehe, akjipepea.punde Mgezi anakuja hadi alipo Nyalwe na kumuambia kuwa chakula kiko tayari. Wanapokaa kula Bokono hali chakula ana wasiwasi sana. Nyalwe anapomuuliza ni kwa nini hali anamjibu kwa kejeli na kumuuliza juu ya vyeo vyake;mke, mwndani na msiri wake. Nyalwe anamueleza Bokono kuhusu ndoto yake .Bokono anakubali kuwa ana hofu ya kunyang’anywa utawala.Nyalwe anamuomba abadilishe mienendo yake na anamuonya dhidi ya vibaraka wake wanoandanganya kuwa anapendwa na Wanabutangi. Bokono anapiga nduru kuwa amamwona nyoka ,anasema ameumwa na bafe lakini wanagundua kuwa hamna nyoka mle ndani ni hofu tu ya Bokono. Nyalwe anampa Bokono habari kuhusu kijiji cha Mama Agoro ambao wangependa kuwagawia huzuni.Hii ni baada ya uwanja wao wa watoto kuchezea umepewa Askari mkuu.Mama Agoro aliahidi kuridi tena na tena kutetea haki yao. Onyesho la tatu Onyeshao hili ni katika gereza. Gereza ni chumba chenye kidirisha kimoja, kuta na sakafu chafu. Tunaonyeshwa mateso na dhuluma kwa Mwelusi kutoka kwa Mweke na Talui. Wanaanza kwa kumita mtukufu mtemi anaponyamaza wanazidi kunchapa na kumsukuma hapa na pale. Mwelusi analalamika kuwa taya zake zinawaka moto kwani waliodai wamekuja kuzungumza naye wanafanya hivyo kwa mateke na makofi. Wanamhoji Mwelusi na kumuuliza kama yeye ni mwelisi wa Biuki na kama anatoka kijiji cha Bunyanya na ukoo wa langile.Anapojibu wanamsifu kuwa yeye ni muungwana na ni kiongozi mzuri sana wa Butangi. Wanamuuliza kama yeye ndiye kiongozi wa kundi la kabakaba.Wanazidi kumchapa ili aliri kuwa anahusika na shughuli za ukombozi lakini Mwelusi anakataa wanazidi kumachapa. Batu anaingia na kuwakataza kumchapa, anaomba nafasi azungumze na Mwelusi. Kwa upole anamshawishi Mwelusi akiri kuwa kiongozi wa wanamapinduzi na aombe msama kwa Mtemi Bokono. Mwelusi anapolia juu ya maumivu Batu anamwambia kuwa atapewa dawa nzuri akitoka gerezani baada ya kuomba msamaha.Batu anamuacha mwelusi peke yake kwani anadai kuwa akili ya binadamu hufanya kazi vizuri akiwa peke yake. Anaporudi na kupata welusi hajafanya uamuzi . Antaka akiri kwamba anatumiwa na majirani ili kuchafua Butangi. Anapotataa Btu anamwambia kuwa amepotoshwa . Batu anatoa ishara kwa Askari na kuondoka. Sura ya nne Onyesho hili linatokea mbele ya gereza.Andua amemletea ndugu yake chakula.Askari wanamkataza kumuona na Askari 111 anajaribu kumdhurumu.Askari wanapanga kula chakula cha mfungwa lakini askari 1 anawakataza na kuwaomba wampe mfunwa chakula chake.anawaambia wenzake kuwa ni walafi.wanazungumza kuhusu utawala wa mtemi Bokono kama utafikia kilele au la. Askari 11 anaeleza jinsi walijaribu kumgeuza mhutumiwa Fulani aache kuwa jiwe awe binadamu.Walimng’oa kucha za mkono na za miguu, walimgeuza kuwa popo na baadaye walifika katikati ya miguu yake na kupiga kambi hapo.badaye walimuua na kumzika msituni. Onyesho la tano. Onyesho hili ni nyumbani kwa Tanyauani.Tanya ameketi akidondoa nafaka katika uteo.Kwenye sehemu nyingine ya ua Gege amekaakaribu na uzio akiukaguakagua.punde anauachilia na kuanza kujishughulisha na utengenezaji wa ala ya muziki. Mamake anamuuliza kwa nini hajaenda kumtizama nduguye, Mwelusi kule gerezani.Gege anwambia mamayake asimzomee.Anaendelea kutengeneza ala na kusema kuwa wasichana watamtambua . Katika kumbukumbu zake Mwelusi anarejea na kumuuliza hali ya uwnaja wa ngoma. Wazungumza kuhusu hali ya wanabutangi.Gege anamshuritisha nduguye kwa kujali jamii kila mara na kusahau maisha yake mwenyewe. Mwelusi anamuomba aieonee huruma Butangi na awe mzalendao. Andua anarejea nyumbani kutoka kisimani.Anajeraha upande mmoja wa uso wake.Anamueleza mam yake kuwa hakupigana mbali amechapwa na Askari. Azena anawatemebelea na kumtuliza Tanay juu ya mwanawe.Anamuomba asife moyo na azidi kumpelekea chakula. Onyesho la sita Onyesho hili ni nje ya gereza pia. Tanya amamletea Mwelusi chakula na pia anataka kuonana naye.Askari wanchukua chakula na kuahidi kuwa watampelekea. Tanya anapowaomba Askari kumwona mwanawe Askari 11 na 111 wanamkazata. Askari 1 anamuhurumia Tanya na kuwaomba wenzake wamkubalie mama huyo kumwona mwanawe. Baadaye Atega analeta chakula zaidi cha mfungwa pamoja na tembo.Askari wanakula chakula hiki na Kumuomba askari 1 ampelekee rafiki yake mkate wa wishwa. Askari 1 anawahadithia juu ya Makea na ulevi wake.Muda huu wote Mwelusi amekuwa akikata minyororo kwa tupa. Baadaye askari 111 napoenda kuchungulia anamwona na kumwita mwenzake atazame pia.Muda kidogo wanasikia umati wa watu .askari wote wanapotea Mwelusi anafunguliw gereza na kupotea. Onyesho la saba Matukio ya onyesho hili ni katika ukumbi wa utawala wa Butangi.Kuna mkutano kati ya Bokono na vibaraka wake.Lengo la mkutano huu ni kupata suluhu la Mwelusi na uchochezi wake. Kame anasema wamuachilie lakini batu anasema hawawezi kumwachilia mhuni.Maoni yake ni kuwa Mwelusi anafaa kuuliwa.Batu anasema kuwa wawandanganye watu kuwa Mwelusi amkufa juu ya ugonjwa wa moyo au aachiliwe kasha njiani apigwe pembe na nyati.Kame anpinga wazo la kumwaga damu ya binadamu. Askari 11 naingia na kuwaarifu kuwa Mwelusi amatoroka gerezani.anapoomba msamaha Batu anamuonya kuwa lazima wamtafute Mwelusi na waijaribu kutoroka kutoka Butangi. Bokono anajiunga nao na anaposikia habari za kutoroka kwa Mwelusi anakasirika na anawaomba wampe heshima yake. Baadaya anawaomba vibaraka wake au wazee wamtafute na kumuua. Batu anatumia Mweke na Talui kumshawishi Gege.Anamwambia amlete pale na kumshawishi.Mweke na Talui wanafanya walivyo ambiwa na Kumwahidi Gege ndoa na Alida baada ya kumuua Mwelusi.Wanajifanya wao ni wavuvi wawili na kuhadithi juu ya ndoa ya Gege na Alida. Onyesho la nane Onyesho ni uani kwa Tanya.Tanya anajishughulisha na kazi za nyumbani.Batu anaingia na kumsalimu.Baada yakuamkiana batu anamwambia kuwa amakuja kwa ziara ya kirafiki. Sitiari ya kozi na njiwa inatolewa na Tanya.Batu anaulizia kuhusu Mwelusi .Hii ndio sababu yake kuja kwa Tanya. Azena anaingia huku akitembea kwa shida.Anasema jinsi walivyovamiwa na mali yao yote kuchomwa.Batu anasema kuwa ni majirani wao waliowavamia lakini azena anasema kuwa ni uongo walivamiwa na wahini wa kulipwa na kina Batu. Tanya na Azena wanajikumbusha nyimbo walizomuimbia Bokono. Mwelusi ana Atega wanatokea na kwa kutumia shingo Tanya anawaelekeza watoroke.Baada ya Batu kutoweka Mwelusi anaeleza mama yake alivyookolewa na umati. Askari wanakuja kwa fujo lakini Mwelusi na Atega wanfaulu kutoroka. Kame anakuja pia na kufikia sasa Tanya anamkejeli kuwa utawala wa Butangi umemtembelea imebaki Bokono Mwenyewe.Kame anawaeleza kuwa nyoyo zao ziko pamoja nay eye ni mmoja wa wanamapindizi.Wote wanaondoka kuelekea kisima cha mkomani aliko Andua na wanamapinduzi wengine. Onyesho la tisa Matukio ya onyesho hili ni kisima cha Mkomani.Ni asubuhi na zigu amesimama huku macho yake yakilikagua bonde.Kaloo anatokea na anapofika karibu na zigu zigu anashtuka.zigu anamuulizia kaloo kuhusu maoni ya wanakijiji wnzake juu ya kannuni mpya zilizotangazwa.Anasema kuwa kanuni zote za Butangi ni za busara. Kaloo anamtuma zigu amshukuru Bokono Kaloo anamtuma zigu amshukuruBokono kwa ajili ya kazi aliyoamuru mototo wake apewe.kaloo hajali juu ya Butangi yeye anataka awe na uhusiano na Bokono ili apate mali zaidi.Kaloo anaambiwa kuwa ni vyema aende akamshukuru mwenyewe kwani hivi karibuni Bokona amekuwa akimtaja mara kwa mara. Andua anapokuta kuteka maji zigu anamkataza na kumueleza kuhusu kanuni.baadaye Mwelusi na Atega wanatokea lakini Zigu hawatambui.Anawazungumzia kuhusu Mwelusi aliye gerezani.Zigu ako tayari kutetea kanuni za Butangi hata kwa silaha. Baadaye Gege anakuja na kumdanganya Mwelusi kuwa ametumwa na mama yao Tanya huku akilia , ni ujumbe muhimu ambazo babayao alimwachia. Wanaenda chemba na Gege anamuua.Kame anafika amechelewa na wote wankimbia chemba baada kusikia sauti yenye huzuni. Onyesho la kumi Matukio ya onyesho hili ni katika Ukumbi wa Utawala wa Butangi.Kiti cha mtemi kiko mahali pake,lakini ni kitupu.Batu ymo ukumbini.Punde Mweke anaingia na baadaye Gege. Wakati Gege anadai malipo yake Baada ya kumuua Mwelusi ndio anagundua kuwa alidanganywa.Batu anamwahidi kuwa atapata zawadi ya ardhi.Bokono anapoingia anamwahidi kuwa atapewa jina Mkuki wa Almasi. Nyalwe anaingia kwa wasiwasi na kuwaonya kuwa umati wa watu unakuja.wanampuuza.Hata hivyo wanashangaa kuwa Mweke hajaleta habari zozote na Zigu pia hakuweko. Azena anaingia ukumbini kama ameinua panga.Kisha askari1,Kame na Atega.Atega anamtetea nyalwe asifungwe kwani alikuwa kamwe anatetea Wanabutangi.Wanawafunga Bokono, Batu,Gege na kuwatoa nje .Watu wanasherekea ukombozi wao. WAHUSIKA Wahusika ni binadamu wa kawaida na wanaendeleza shughuli za kawaida za kila siku za binadamu. Mhusika mkuu ni Mwelusi .Ni kiongozi katika shughuli za ukombozi wa butangi.Anafungwa katika jela na kuteswa sana.(uk 21) onyesho la tatu. Gege ni nduguye Mwelusi yeye anaendleza maudhui ya ubinafsi.Hana utu,ni msaliti na pia muuaji kwani alimmuua Mwelusi pale kisimani. Bokono ni kiongozi mbaya mwenye udikteta.Ananyanyasa na kukandamiza Wanabutangi.Anawanyima wanabutangi haki zao Kupitia vibara wake Batu na Zigu.Viongozi hawa ni wakatili,hawana utu. Wanamdanganya Bokono kwamba anapendwa lakini huo ni unafiki wao. Tanya na Azena ni wanawake wanao tetea haki za wanabutangi.Tanya ni Mamake mwelusi na nimkakamavu anazozana na Batu na habadilish msimamo wake.Uk 76 onyesho la nane. Atega na Andua ni wasichana ambao wanashiriki katika ukombozi ni wakamavu, wana ujasiri na pia ni wenye nidhamu hasa Atega kwa kuwapa askari tembo na kumpelekea Mwelusi tupa.Hawa ni wahusika wasaidizi. Kuna wahusika wengi kama vile Askari 11 na 111ambao wanaendeleza maudhui ya ukatili na dhuluma pamoja na Mweke na Talui. Kame na Askari 1 ni wenye utu na wamezinduka na kushiriki katika ukombozi. Kaloo ni kibaraka wa Mtemi Bokono.Yeye hajazinduka.Ni mwenye ubinafsi na anamtetea mwanawe.Ni mfisadi MANTHARI Ni mahali au mazingira yanayotumika katika kitabu. Mazingira ya kawaida yametumika katika tamthilia hii.Kuna mazingira ya kinyumbani kama vile Kwa Tanya, Nyumbani kwa Bokono uk 12 onyesho la pili.Kuna mazingira ya uwanjani, kisimani na gereza. MBINU ZA UANDISHI NA ZA LUGHA Kejeli uk 21 Mweke na Talui wanawita Mwelusi Mtukufu Mtemi.Hii ni kejeli kwani Mwelusi si mtemi mbali ni kiongozi wa ukombozi.Kejeli inasaidia kuendeleza maudhui ya dhuluma. Matumizi ya Ndoto uk 14 Nyalwe mkewe Bokono antuhadithia jinsi usiku mmewe alikuwa akiota na kusema watu wamtoe kaburini. Ndoto hii inaonyesha hofu ya Bokono kutokana na utawa wake ambao ni mbaya.Ndoto hii inaendeleza maudhui ya Hofu na utamaushi. Kuna Nyimbo uk 81Azena na Tanya wanakumbuka nyimbo za kumsifia Bokono. Wimbo huu unaonyesha Bokono kama kiongozi bora asiye na kasoro.Wanabutangi waliimuinua Bokono karibu na mungu.Maudhui yake ni ya uongozi wa kidkteta. Kuna matumizi ya Taswira.Hizi ni picha zinazojengeka katika akili ya msomaji.Mwandishi ametumia taswira mbalimbali kama vile gereza.Uk 21 gereza imechorwa kama mahali penye kidirisha kimoja ,kuta na sakafu chafu. Picha hii inasaidia kuendeleza maudhui ya dhuluma na kunyimwa haki kwa mfungwa. Takriri imetumika uk 6 ambapo Kaloo, Azena na Gege wanakariri Bokono Bokono Milele mara kadhaa.Hii inasaidia kumpa Bokono matumaini ya kuwa anapendwa.Huu ni Unafiki.Kuna takrir pia katika kurasa zifuatazo uk 8,11,14 Tashhisi imetumika katika ukurasa wa kwanza ambapo sauti inasema kuwa jua lina bahati,jua lina uwezo uwezo mkubwa. Mwelusi pia anasema mawazo yamemshika miguu kuonyesha hofu aliyonayo.askari wanasema kuwa siku inajikokota. Uk 53.Hii inaonyesa ukatili wao na dhuluma na mateso wanayomletea mwelusi. Andua anaambiwa na Askari asipoondoka atatemebelewa na makofi.Hii ni dhuluma. Tashbihi ni ulinganisho wa moja kwa moja wa vitu au watu na wanyama. Mfano uk71Alida bintiye mtemi ana shingo ya upanga.Hii ni kusaidia kumshawishi Gege na maelezo haya yanaendeleza unafiki kwani ndoa anayoahidiwa na hurulaini haipo. Uk 37 Askari wanasema uharibifu wa mwelusi uko wazi kama meno ya ngiri. Jazanda ni picha inayomwingia mtu akilini na kuilinganisha na hali ya kawaida.Mfano uk 61 Batu anaashiriwa kama macho na masikio ya Butangi, uk64 mwelusi ni mwiba wa Butangi.Hii ni tofauti na jukumu lake la kuleta mabadiliko katika utawala wa Butangi lakini si kuzuuia maendeleo. Methali mfano uk55 Batu anasema kuwa dawa ya moto ni moto. Hii ni katika hatua aliyochukua ya kutumia watu kuvamia kina Azena.Huu ni ukatili wa kiwango cha juu. Methali pia zimetumika katika kurasa zifuatazo 16,52,39,102 na kadhalika Chuku ni kutia chumvi au kuongeza sifa ili jambo au kitu kiwe cha kuvutia. Mfano uk 71 Maelezo ya Alida yametiwa chumvi ili kumvutia Gege. Katika uk 9 baada ya mambo kutulia na hasira ya mtemi Bokono Kuisha Batu,Zigu,Kaloo, Azena na wengine waliofika wanaanza kumsifia Bokono ;Utaongoza Butangi kwa miaka mia moja.Hii ni chuku kwani Mtemi ameshazeeka na hawezi kutawala kwa miaka mia moja. Chuku pia imetumika katika kurasa zifuatazo 30,72,56 na kadhalika. Semi uk27 Mwelusi anasema koo lake liko motoni.Hii ni baada ya kichapo na mateso anayopata gerezani.Semi hii imetumika kuonyesha dhuluma na mateso kwa Mwelusi. Askari 11 anaeleza jinsi walijaribu kumgeuza mhutumiwa Fulani aache kuwa jiwe awe binadamu.Walimng’oa kucha za mkono na za miguu, walimgeuza kuwa popo na baadaye walifika katikati ya miguu yake na kupiga kambi hapo.Inamaanisha kuwa walimvuta na kumkata na kumdhulumu sehemu zake za siri. Semi pia zimetumika katika kurasa zifuatazo 15.27,37 na kadhalika Mwandishi ametumia Lugha ya Matusi. Hasa katika mazungumzo ya Bokono na Nyalwe.Mfano mwehu MAUDHUI Mambo muhimu yanayoelezwa katika tamthilia.Mwandishi ameshighulikia maudhu kuu kama vile uongozi mbaya, dhuluma na mateso,ubinafsi na ukombozi.maudhui mengine ni kama vile usaliti, ubinafsi, utu, unafiki na uchochezi. Uongozi Mbaya Mtemi wa Butangi Bokono pamoja na vibaraka wake Batu na Zigu wanaendeleza maudhui ya uongozi mbaya. Wanamfanya Mwelusi kukamatwa na kufungwa gerezani bila makosa yoyote amabayo wanaweza kuthibitisha. Katika Mkutano batu anaeleza jinsi walichoma kijiji cha Kina Azena na kusema mfumo wake wa uongoni ni dawa ya moto ni moto. Kwa kuwa Mwelusi anatetea haki za wanyonge Bokono anamwita mwiba. Hii ni kwa sababu anazuia yeye na vibaraka wake kujichumia mali. Mwishowe wanamtumia Gege kumuua. Wanaamua kuwanyima Wanabutangi haki ya kuteka maji pale kisimani. Mtemi anauliza kamawamewatangazia watu kuhusu kanuni mpya ya kuteka maji kisima cha Mkuyuni kuwa ni siku tatu kwa wiki. Dhuluma Na Mateso Askari 11 anaeleza jinsi walijaribu kumgeuza mhutumiwa Fulani aache kuwa jiwe awe binadamu.Walimng’oa kucha za mkono na za miguu, walimgeuza kuwa popo na baadaye walifika katikati ya miguu yake na kupiga kambi hapo.badaye walimuua na kumzika msituni.uk 43 Mwelusi anafungwa gerezani kama hakuna kesi na hajahukumiwa.Batu anapomtemebela baada ya kumshawishi akiri kutochochea Wanabutangi na kushindwa anawaagiza Askari wazidi kumchapa na kumtesa.uk 29 Katika uk 30 Mwelusi anasema anachomwa na mikuki mia moja na anaelezwa kama anayeumia.Hii ni kutokana na kichapo anachopata kutoka kwa Askari. Uk49 Andua anasema kuwa hakupigana alipigwa na ndia sababu ako na jeraha upande mmoja wa uso wake.Anasema kuwa ni Ni Askari waliwapiga kule kisima cha Mkuyuni baada ya wao kwenda kuteka maji. Askari wa Butangi kulingana na Tanya si wa kulinda mbali ni wa kuleta mateso na kuwachapa Wana butnagi. Tanya anasema kuwa juzi walimngoa motto wa Chendeke meno. Uk 24 Mweke na Talui wanapokuja kuzungumza na Mwelusi wanafanya hivyo kwa makofi na mateka.Mwelusi anasema kuwa taya zake zinawaka moto. Batu anajaribu kuukinga uongozi wa Bokono na amamuomba mwelusi kuacha uchochezi na kuomba msamaha.Mwelusi anapokataa kukiri kwamba anatumiwa na majirani ili kuchafua Butangi. Anapotataa Batu anamwambia kuwa amepotoshwa . Batu anatoa ishara kwa Askari na kuondoka. Yeye anawpa ruhusa Askari wamtese mwelusi badala ya kumlinda.uk 36 Ubinafsi Tunauona ubinafsi wa Gege .Uk wa 95 Gege anamuua Mwelusi nduguye ili apate kuozwa Alida bintiye Mtemi. Uk 17 anamuambia Mwelusi ajali maisha yake aachane na jamii. Gege hajali maisha ya wnabutangi wengine anajijali yeye mwenyewe. Uk 89 Kaloo anamtuma zigu kwa Bokono amshukuru kwa ajili ya kazi aliyoamuru mototo wake apewe.kaloo pia hajali juu ya Butangi yeye anataka awe na uhusiano na Bokono ili apate mali zaidi. Gege hajaenda kumtizama nduguye, Mwelusi kule gerezani.Gege anwambia mamayake asimzomee anapoulizwa.Anaendelea kutengeneza ala na kusema kuwa wasichana watamtambua .Hivyo anajali sana wasichana kuliko nduguye.uk43 Ukombozi Mwelusi,Atega.Andua,Kame na Askari 1 ni baadhi ya wanamapinduzi katka Butangi. Watu hawa wanapinga utawala wa Mtemi Bokono na vibaraka wake. Wakati Mwelusi amefungwa gerezani Atega anamletea mkate wa wishwa ukiwa na tupa ambayo anatumia kukata minyororo na kujikomboa. Baadaye umati wa watu wanakuja na kumsaidia kufungua gereza na kujikomboa.uk 59 Kwa Uongozi wa Mwelusi wanaendelea kutetea haki zao.Mfano Andua anaenda kisimani kuteka maji. Hata baada ya mwelusi kuuliwa na Gege wanamapinduzi hawa wanaendelea na harakati zao za ukombozi. Uk 105 Kitabu kinaisha kama Bokono,Batu,Zigu , Mweke na Gege wamefungwa kamba baada ya kufumaniwa na Waandamanaji.Hivyo wanaukombozi wanafaulu kukomboa Butangi kutokana na utawala Mbaya. Mwelusi anadaiwa kuwa yeye ndiye kiongozi wa kundi la kabakaba. Anahusika na shughuli za ukombozi.Ni yeye kiongozi wa kundi hili la wanamapinduzi. Usaliti Gege anamsaliti kakake, Mwelusi kwa Kumuua pale Kisimani. Uk 95 Gege anamdanganya Mwelusi kuwa ametumwa na mama yao Tanya huku akilia , ni ujumbe muhimu ambazo babayao alimwachia. Wanaenda chemba na Gege anamuua. Viongozi wa Butangi ikiwemo Batu na Zigu wanawasaliti kwa kuwanyima haki zao na kuwatesa. Utu Kame Askari 1 ni wenye utu wanamtetea Mwelusi. Uk 60 wakati Batu na zigu wanataka kumuua Mwelusi Kama anasema wamuachiliea kwa kuwa hana makosa yoyote. Uk 35 Tanya anapowaomba Askari kumwona mwanawe Askari 11 na 111 wanamkazata. Askari 1 anamuhurumia Tanya na kuwaomba wenzake wamkubalie mama huyo kumwona mwanawe. Hawa wawili paoja na wengine kama vile Azena na Atega ni wenye utu miongoni mwa wanabutangi wengi ambao wana unyama kama vile Batu. Askari wanapanga kula chakula cha mfungwa lakini Askari 1 anawakataza na kuwaomba wampe mfunwa chakula chake.uk 37 Unafiki Uk 25 Mweke na Talui wanamhadithia Gege jinsi harusi yake na Alida itakavyokuwa. Wanamwambia Gege amuue Nduguye Mwelusi na atapewa mali pamoja na kuoa mtotot wa Mtemi Bokono. Wakati Gege anaenda kudai malipo yake Baada ya kumuua Mwelusi ndio anagundua kuwa alidanganywa.Talui na Mweke ni wanafiki walijua kuwa wanamdanganya Gege ili awasidie tu kumumaliza Mwelusi. Batu anapomtemebelea Mwelusi gerezani anamwambi a kuwa ni rafiki yake na kumuomba ajiunge naye katika kuitumikia Butnangi.Huu ni unafiki kwani kabla ya hapo alipokuwa kwenye mkutano na Zigu na Kame alpanga jinsi watakavyo muua. Uk 79 Batu anapomtembelea Tanya anamwita rafiki yake tangu ujana wao.huu ni unafiki kwani Batu yuko pale kumtafuta Mwelusi. Baada ya kumuahidi Tanya kuwa watampa Mwelusi chakula Askari wanakula chakula hiki na Kumuomba askari 1 ampelekee rafiki yake mkate wa wishwa. Uk 58. Huu ni unafiki. Uchochezi Kabla mkutano uanze Mwelusi anafika pale na kudai kuwa anapita.Hata hivyo nia yake wakiwa na Atega ni kuwachochea watu wasuhudhurie mkutano wa Mtemi Bokono.Uk 1 Uk wa 9 Zigu anasema kuwa kuna fununu ya kuwa kuna kijana anayechochea watu.Kijana huyu ni Mwelusi. Uk 90 Zigu anamwambia Kaloo kwamba Bokono amekuwa akimtaja mara kwa mara.Zigu ananchochea Kaloo aonane na Bokono na kumpa shukrani yeye mwenye kwa kazi ambayo Bokono alamuru motto wa Kaloo apewe. FALSAFA YA MWANDISHI Mwandishi analenga kuzindua wananchi kuhusu utawala mbaya.Anatetea haki za walionyanyaswa na kukandamizwa. Anashikila kuwa kuna uwezo wa kujikomboa kutoka kwa uongozi mbaya .Hii ni kupitia kwa watu kuungana na kuandama na kutetea haki zao na kubadilisha uongozi mbaya ,pamoja na kuwafungaviongozi wabaya. Falsafa ya Kithaka ni haki na hukumu kwa wenye makosa. NADHARIA Mwandishi ametumia Nadharia kama vile Umaksi.Katika Butangi wenye mali wananyanyasa wasio na mali.Kuna Ufeministi kwani Atega ,Andua Tanya na Azena ni wahusika wa kike wanaoshiriki katika ukombozi.Kuna Uhalisia Kwani matukio ni ya kawaida kam vile uongozi mbaya na kunyimwa haki katika maisha ya kila siku. Kuna Utamaushi kwani wanabutangi wamekata tama.Mfano Tanya anamtaka Mwelusi aondoke Butangi HITIMISHO Mwandishi amefaulu kutumia mbinu na kutoa maudhui kwa kutumia nadharia. Kithaka anatetea haki kwa wenye Kunyanyaswa na hukumu kwa wenye makosa.Amewatumia wahusika wa kawaida kuutoa ujumbe wake. Kuna udhaifu katika anwani kwani sio wahusika wote wanaathiriwa na kifo kisimani.Kitabu kimeshughulikia zaidi ya kifo. UHUSIANO KATI YA TAMTHILIA YA KIFO KISIMANI NA UTENZI W A FUMO LIYONGO Utenzi wa fumo liyongo unamhusu shujaa Liyongo kutoka jamii ya waswahili.liyongo alishuhudiwa na jamii yake na makabila jirani kama vile wagalla. Hata hivyo mfalme wa pate(Daudi Mringwari) alimchukia kwa kuhofu kuwa angemnyang’anya utawa wake.Hivyo alipanga njama za kumwangamiza liyong.Akamtia gerezani alikolindwa na Askari wake.Akiwa gerezani, aliletewa mkate wa wishwa uliotiwa tupa.Aliitumia tupa hii kukata minyororo kasha akotoroka. Mfalme wa pate hakukata tama.Alimshawishi mwanawe Liyongo kumuua babake na kumwahidi kumwoza bintiye.Liyongo akauliwa na mwanawe kwa kumfuma msumari wa shaba kitovuni.Liyongo alifia kisimani na kuwatisha watu wasichote maji kwa siku kadhaa. Utenzi huu kwa kiasi kikubwa unahusiana na tamthilia ya Kifo Kisimani, inayomhusu Mwelusi anayepinga utawala dhalimu wa Mtemi Bokono. Anachukiwa na Bokono pamoja na vibaraka wake kwa hofu kuwa atauangusha utawala huo.Anatiwa gerezani lakini anatoroka baada ya kukata minyororo kwa tupa iliyotiwa ndani ya mkate wa wishwa alioletewa na Atega. Bokono anamtumia nduguye Mwelusi, Gege kumuua kwa kumdunga kisu pale kisimani. Gege vilevile anaahidiwa na Mweke wakiwa na Talui kuwa ataozwa bintiye mtemi.Alida. Hata hivyo kuna tofauti nyingi kati ya tungo hizi mbili. Fumo Liyongo ni mhusika wa kihistoria, aliishi baina ya karne 15 na 16.Mwelusi naye ni mhusika wa kubuni.Fumo alikuwa na sifa za kiajabu kama vile nguvu zilizokithiri, mpiganaji hodari aliyeshinda vita vingi, ukubwa uliopita kiasi na uwezo wa kutambua mabo kabla hayajiri.Mwelusi hana sifa kaa hizi zinazomtambuliasha kama mhusika wa kipekee.Vita anavyopigana si vya silaha bali anapinga dhuluma na mateso kwa Wanabutangi. MAREJELEO. 1. Kithaka wa Mberia, (2001) Kifo Kisimani, Marimba Publications limited, Nairobi Kenya. 2. Rocha M.Chimera, (1998) Kiswahili; Past, Present and Future Horizons,Nairobi University Press,.Nairobi. 


Friday, 29 July 2016

sajili katika lugha

Sajili 
Ni matumizi ya lugha katika muktadha mbalimbali.Kuna sajili anuwai za matumizi ya lugha katika jamii. Hapa tutazingatia mifano michache ya sajili mbali mbali.Kila sajili huwa na sifa mbalimbali zinazoitofautisha sajili hiyo na nyinginezo. Ili kubaini sifa za lugha katika sajili fulani, ni muhimu kuzingatia baadhi ya maswali yafuatayo:
·      ni mazungumzo baina ya nani na nani?
·      kuna uhusiano gani baina ya wanaozungumza?
·      yanapatikana wapi?
·      yanatumika katika hali gani?
·      yana umuhimu ama lengo gani
·      ni istilahi zipi istilahi (maneno maalum) zinazopatikana katika mazingira hayo?
·      umaizi wa lugha baina ya wazungumzaji ni wa kiwango gani?
·      ni mtindo gani wa lugha unaotumika?
Sajili ya Ajali

Hii ni lugha inayotumiwa katika ambalo ajali imetokea. Wahusika wanaweza kuwa majeruhi, polisi, walioshuhudia au wananchi wengine n.k
Sifa za lugha inayopatikana katika sajili hii
1.  Msamiati wa kipekee unaohusiana na ajali kama vile majeruhi, hudumanya kwanza, damu, mkasa.
2.  Hutumia lugha ya kudadisi dadisi ili kubaini chanzo cha ajali.
3.  Huwa na masimulizi – walio na habari kuhusu kisa hicho hueleza waliyoshuhudia
4.  Kutokana na hali ya msukosuko, lugha hii haina utaratibu – watu huwa katika hali ya hofu, kwa juhudi za kuwaokoa majeruhi.

Mfano wa Sajili ya Ajali
Mwanakijiji 1:
Nimesikia twa! Kisha kishindo kikubwa sana (akihema hema) Nikaambia kuna mlipuko tukimbie.
Mwanakijiji 2:
Lilio la muhimu ni kuyaokoa maisha ya majeruhi kwa kuwapa huduma ya kwanza.
Mwanakijiji 1:
Tuondoeni miili ya waliofariki kwanza.
Mwanakijiji 2:
hatuwezi kuishika miili iliyobanwa katika gari hadi polisi wafike. Na ndio hao wanaokuja!
Mwanakijiji 1:
(akikimbia) Ndio hao! Acheni kuiba mafuta! Polisi wanakuja!
Polisi:
Wakitawanya wananchi walioliparamia gari kuiba bidhaa mbali mbali.Liinueni hili gari! Wapi dereva?
Dereva:
(ambaye amelala akihema kwa maumivu, damu ikichuruzika miguuni na mikononi) Nilisitishwa na ng'ombe waliokuwa wakivuka barabara. Nilijsribu kukwepa lakini usukani ukanishinda gari likapoteza mwelekeo…
Abiria:
Alikuwa akiendesha gari kwa kasi sana. Tukampigia kelele apunguze mwendo lakini hakutusikia. Matunda yake…
Mwanakijiji 2:
Niliona gari likibingiria mara kadhaa mpaka likaingia humu mtaroni, ndiyo tukakimbia kuwaokoa.
Polisi:
Nyamazeni! Achieni polisi kazi iliyobaki. Ikiwa kuna yeyote anayejuana na waathiriwa aandamane nasi.
Sajili ya Biashara

Lugha ya biashara huzungumzwa na wauzaji na wanunuzi katika sehemu za kibiashara. Inapaswa ikumbukwe kwamba lugha hii inaweza kubadilika kidogo kulingana na mazingira. Kwa mfano, katika mikutano ya kibiashara, lugha rasmi hutumiwa ilihali katika soko, lugha ya mitaani inaweza kutumika.
Sifa za Lugha ya Biashara

1.  Hutumia msamiati wa kibiashara kama vile:
·      Fedha
·      Faida
·      Hasara
·      Bei
·      Bidhaa
2.  Hutumia misimu ili kuwavutia wanunuzi
3.  Ni lugha yenye malumbano hasa watu wanapojadiliana kuhusu bei
4.  Ni lugha legevu - haizingatii kanuni za lugha.
5.  Huchanganya ndimi kwa kuingiza maneno ya lugha za kigeni
6.  Ni yenye heshima na unyenyekevu kwa wanunuaji
7.  Msamiati katika lugha ya Kibiashara
Mfano wa Sajili ya Biashara

Mtu X:
Tatu kwa mia! Tatu kwa mia! Leo ni bei ya hasara!
Mtu Y:
Unauza hii briefcase kwa pesa ngapi?
Mtu X:
Hiyo ni seventy bob mtu wangu
Mtu Y:
Huwezi kunipunguzia. Niuzie hamsini hivi.
Mtu X:
Haiwezekani mtu wangu. NItapata hasara nikiuza hivyo. Ongeza mkwaja, mama.
Mtu Y:
Basi hamsini na tano.
Mtu X:
Tafadhali ongeza kitu kidogo. Unataka nikule hasara leo? Fikisha sitini na tano.
Mtu Y:
Basi sitanunua hii. Sina pesa hizo zote. Unajua uchumi ni mbaya siku hizi.
Mtu X:
Tafadhali mtu wangu. Huu mkoba ni mzuri sana. Umetoka Germany. Angalia. Unaweka pesa hapa, kitambulisho hapa halafu unafunga hivi. Hauwezi kupoteza chochote ukiwa na mkoba huu. Angalia wewe mwenyewe. Hakuna mahali pengine utaweza kununua mkoba huu kwa bei ghali kama hii.
Mtu Y:
Nimekwambia sina hizo pesa. Nitanunua baadaye ukipunguza bei.
Mtu X:
Lete sixty bob. Lakini utakuwa umeniumiza. Nakufanyia hivyo kwa kuwa wewe ni customer poa.
Mtu Y:
Sawa basi nitanunua. Shika sixty bob.
Mtu X:
Asante Customer. Mungu akubariki. (akimfungia) Hey! Tatu kwa mia. Bei ya hasara! Tatu kwa mia!
Sajili ya Bungeni

Hii ni lugha inayozungumzwa wakati wa kikao cha bunge. Sajili hii ni tofauti na na sajili ya siasa, ambayo huhusisha wanasiasa wakipiga kampeni.
Sifa za Lugha ya Bungeni

1.  Ni lugha yenye ushawishi – wabunge hutumia vishawishi ili kuwahimiza wenzao waunge ama kupinga msalaba
2.  Ni lugha ya mjadala yenye waungao na wapingao.
3.  Ni lugha yenye heshima na nidhamu. Maneno ya heshima kama mheshimiwa, tafadhali na samahani hutumika sana.
4.  Hutumia maneno maalum yanayopatikana katika mazingira ya bunge kama vile kikao, mswaada, kuunga mkono, kujadili, kupitisha, n.k.
5.  Lugha ya bungeni ni rasmi na sanifu.
6.  Hulenga maswala mbalimbali ya kisiasa na maendeleo katika taifa.
7.  Huwa na maelezo kamilifu
8.  Ni lugha yenye maswali na majibu miongoni mwa wabunge.

Mfano wa sajili ya Bungeni
Spika:
Waheshimiwa, muda unayoyoma. Nawaomba mfanye mazungumzo yenu sauti ya chini tumsikize huyu. Endelea mheshimiwa.
Mbunge 1:
Asante Bwana spika. Hii siyo mara ya kwanza ya kuuwasilisha mswaada huu hapa. Kila mbunge anayethamini raia wa taifa hili ni lazima auunge mkono mswada huu. Katika kikao kilichotangulia, mliupinga mkidai kwamba hauna heshima kwa rais. Leo tumefanya ukarabati wote mliotaka. Hamna budi kuuunga mkono. Bwana spika….
Spika:
Muda wako umekwisha tafadhali keti. Wabunge wataamua hatima ya mswada huu ikiwa utapitishwa kama sheria. Lakini kumbukeni uamuzi wa mwisho ni wa rais
Sajili ya Hospitalini

Hii ni lugha ambayo huzungumzwa katika hospitali baina ya madaktari, wagonjwa, wauguzi n.k
Sifa za Lugha ya Hospitalini
1.  Hutumia msamiati wa hospitalini kama vile
·      dawa
·      magonjwa
·      Daktari
·      Wadi
·      Mgonjwa
·      Dawa
·      Kipimo
2.  Ni lugha yenye upole na heshima
3.  Huwa na maswali mengi hasa daktari anapotaka kutambua kiini cha ugonjwa unaomhadhiri mgonjwa wake
4.  Ni lugha yenye hofu na huzuni

Mfano wa Sajili ya Hospitalini
Daktari:
Ulianza kuumwa hivi lini?
Mgonjwa:
Kichwa kilianza kuniuma jana jioni baada ya chajio. Nilipoamka asubuhi nikatambua kwamba hata tumbo lilikuwa likiuma pia.
Daktari:
Ulipoanza kuumwa na mwili mzima, ulichukua hatua gani? Hukunywa dawa yoyote?
Mgonjwa:
Nilichukua tembe zilizokuwa zimepatiwa kakangu miaka mitano iliyopita alipokuwa akiumwa na malaria.
Daktari:
Kila ugonjwa huitaji matibabu mbalimbali. Tembe za malaria haziwezi kutumika kutibu maumivu ya kichwa na tumbo. Pia ni hatari kutumia dawa ambazo zimepitwa na wakati. Zinaweza kukuletea madhara zaidi.
Mgonjwa:
(akikohoa) Sijui kama una tembe za kifua pia. Hii baridi inaniletea homa mbaya.
Daktari:
Hatuwezi kukupatia dawa kabla ya kutambua ugonjwa ulio nao. Itabidi tupime joto lako, damu na pia mate yako ili kupata tatizo linalokusumbua. Kisha tutakupatia dawa. Je, una umri wa miaka mingapi?
Mgonjwa:
Nikichukua hizo dawa nitapona?
Daktari:
Matokeo hubadilika kutoka kwa mgonjwa mmoja hadi mwengine. Inaweza kuchukua muda. Huenda ukalazwa kwenye wadi kwa siku mbili tatu hivi. Umri wako, mama?
Sajili ya Kidini

Katika sajili ya kidini tunaangazia lugha inayozungumzwa na waumini/washiriki wa imani fulani wakati wa ibada, sala, katika nyumba takatifu au mahali popote pale ambapo wanazungumzia mambo yanayorejelea imani au Mwenyezi Mungu.
Sifa za Lugha ya Kidini

1.  Hutumia msamiati wa kidini kama vile
·      Bibilia
·      maombi
·      mbinguni
·      jehanamu
·      Madhabahu
·      Paradiso
·      Mbinguni
·      Mwenyezi Mungu
·      Mwokozi
2.  Ni lugha inayonukuu sana hasa wazungumzaji wanaporejelea Kitabu kitakatifu
3.  Lugha yenye heshima, upole na unyenyekevu
4.  Lugha sanifu
5.  Ni lugha iliyojaa ahadi nyingi kwa wanaoandamana na mafunzo ya kidini na vitisho kwa wanaoenda kinyume na mafundisho
6.  Huwa imejaa matumaini
7.  Ni lugha yenye kutoa maneno ya sifa, kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu

Mfano wa Sajili ya Kidini
Boriti:
Bwana asifiwe Bi...
Bi Rangile:
Amina, mchungaji. Watoto wanaendeleaje?
Boriti:
Karita hana neno. Mwenyezi Mungu ametunyeshea rehema na neema zake. Je, wajukuu wako wa hali gani?
Bi Rangile:
Wanaendelea vizuri isipokuwa hawataendelea na masomo. Sijui nilimfanyia Mungu dhambi gani.
Boriti:
Nasikitika sana kusikia hivyo. Mungu atawalinda mayatima hao. Yeye ndiye baba wa mayatima. Mungu ni mwenye huruma.
Bi Rangile:
Sijui hayo, mchungaji. Hata sijui maana ya kuishi hapa duniani. Kila siku ni matatizo.
Boriti:
Usife moyo. Mungu anasema katika kitabu cha Yohana 14:18, "Sitawaacha nyinyi kama mayatima..." Kwa hivyo, ukiwa na imani, Mungu atakuonekania.
Bi Rangile:
Basi niombee mchungaji ili Saumu na Neema wapate karo ya kurudi shuleni.
Boriti:
Funga macho tusali. Ewe Rabuka uliyejaa neema na baraka tele. Tunakushukuru na kulitukuza Jina lako takatifu kwa baraka zako za ajabu. Tunajua kwamba wewe ndiye Mungu uliyewatoa wana wa Israeli kutoka Misri. Sisi wenye dhambi tunakuja mbele yako tukiomba ukafanya miujiza katika nyumba hii ya Bi Rangile......
Wote:
Amina.
Sajili ya Kisayansi

Sifa za Lugha katika sajili hii
1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaoambatana na taaluma inayorejelewa.
2.  Huwa na maelezo kwa ukamilifu.
3.  Huwa na mpangilio maalum na maendelezo ya hoja na ujumbe.
4.  Huchanganya ndimi na kutumia maneno ya kisayansi au lugha mbalimbali.
5.  Hutumia lugha sanifu.
6.  Ni lugha yenye udadisi mwingi (wakati wa kufanya utafiti)
Kwa sababu zisizoweza kuepukika, kikundi chetu hakitamaliza utafiti ulioratibiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi ujao. Hii ni kwa sababu ya changamoto kadhaa ambazo tumekutana nazo. Kwanza, viluwiluwi, ambao ndio tunaotafiti wamekuwa haba sana wakati huu wa ukame. Pili, kutokana na kufungwa kwa maabara ya kisayansi katika taasisi hii, ni muhali kufanya majaribio yoyote ya kazi yetu. Tatu, kumekuwa na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya wanakijiji kwamba kukusanya viluwiluwi kunawatia hofu. Aidha, tume yetu imepungukiwa na fedha baada ya serikali kusitisha kudhamini utafiti huu.
Baada ya kujadiliana kwa vikao tatu mfululizo, tume yetu inapendekeza haya: Muda wa kufanya utafiti uongezewe kwa kipindi cha miezi sita; serikali kupitia kwa taasisi hii ifadhili wachunguzi. Wananchi wahamasishwe kuhusu umuhimu wa kuwafanyia viwavi utafiti na maabara ya utafiti ikaraatiwe haraka iwezekanayo.
Sajili ya Mahakamani

Hii ni lugha inayozungumzwa na wanasheria, mahakimu, mawakili, washitakiwa na mashahidi katika mahakama.
Sifa za Lugha ya Mahakamani

1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaorejelea sheria kama vile
·      katiba
·      sheria
·      mashtaka
·      Hakimu
·      Ushahidi
·      Wakili
·      Jela
·      Mshitakiwa
·      Kiongozi wa mashtakiwa
2.  Huwa na maelezo marefu na ya kina ili kutafuta ushahidi wowote uliopo
3.  Ni lugha yenye kunukuu sana hasa vipengele katika vitabu vya sheria kama vile katiba
4.  Ni lugha rasmi na sanifu
5.  Ni lugha iliyojaa maswali na majibizano
6.  Ni lugha yenye heshima

Mfano wa Sajili ya Mahakamani
Kiongozi:
Musa Kasorogani, mwanaye Bi Safina na Mzee Mpotevu Kasorogani; umeshtakiwa kwa kosa la jaribio la mauaji mnamo tarehe 23/08 mwaka huu. Unaweza kukubali mashitaka, kukana au kunyamaza. Je, unakubali mashitaka.
Musa:
Naomba kukanusha mashtaka hayo, bwana mkubwa.
Kiongozi:
Je, kuna shahidi yeyote katika kesi hii?
Katili:
Hapa mkubwa. Siku hiyo ya tarehe 23/08, Musa alipatikana akiwa akijinyonga usiku wa maneno. Kijiji chote kilikusanyika hapo kwenye boma ya Kasorogani. Nilipoleta polisi, wakamkamata na kumpeleka hospitalini atibiwe kwanza. Ndiposa ameletwa hapa siku ya leo.
Kiongozi:
Je, mshitakiwa una tetesi lolote. Ama pia unaweza kuleta wakili wako azungumze kwa niaba yako.
Kisaka:
Bwana mkubwa, mimi ndiye wakili na shahidi wa Musa. Musa hakuua mtu. Alikuwa akijinyonga kutokana na mkasa uliomfika tarehe hiyo ya Agosti 23 baada ya bibi harusi wake kubadilika. Mimi na mamake, Bi Safina Kasorogani tulijaribu kumtuliza jioni hiyo. Asubuhi nilipoamka siku iliyofuatia, nikapata habari kwamba alikuwa amepelekwa hospitalini. Je, alipojaribu kujiua, alimwua mtu yeyote?
Kiongozi:
Kulingana na katiba ya nchi hii, kifungu cha 12.ab, kuua ni kutoa uhai wa binadamu yeyote. Haijalishi ikiwa ni yeye mwenyewe au ikiwa ni rafiki yake. Hivyo basi jaribio la kujiua ni hatia kulingana na kanuni za nchi hii. Una jingine la kuulizia?
Kisaka:
Je, sheria yetu inaruhusu mtu kuadhibiwa kwa kosa ambalo hakufanya?
Kiongozi:
La hasha.
Kisaka:
Basi tutakuwa tumekiuka kanuni za nchi yetu iwapo tutamhukumu Musa kwa kujiua ilhali hakujiua bado. Tunawezaje kutambua kama angekufa?
Katili:
Inafaa ahukumiwe kinyonga au kifungo cha maisha gerezani. Hata alivunja simu yangu...
Kiongozi:
Order! Lazima kutii mpangilio wa mahakama. Katili hauruhusiwi kuongea bila ruhusa ya hakimu au kiongozi wa mashitaka. Polisi, mpelekeni nje.
Sajili ya Matanga

Ni lugha inayotumiwa katika shughuli za mazishi au nyumbani kwa marehemu.
Sifa za Lugha ya Matanga/Mazishi

1.  Hutumia msamiati wa maneno ya huzuni kama vile waombolezaji, makiwa, kifo, mauti, pole n.k.
2.  Hutumia lugha ya kuliwaza/kufariji na kupa matumaini hasa kwa waombolezaji.
3.  Ni lugha yenye unyenyekevu isiyotumia maneno yanayokera.
4.  Hudhihirisha unyonge wa mwanadamu, kama asiye na mamlaka juu ya uhai wake.
5.  Huwa na mbinu rejeshi kurejelea maisha ya marehemu alipokuwa hai.
6.  Kwa mara nyingi hutumia maneno ya kusifu marehemu kutokana na aliyotenda.
7.  Wakati mwingine huwa ni lugha inayodhihiri hali ya kukata tamaa.

Mfano wa Sajili ya Matangani
"Waombolezaji wenzangu, kama mnavyojua tumekusanyika hapa kwa ajili ya kumsindikiza rafiki yetu amabye amelala hapa. Ikiwa kuna mtu alifikwa zaidi na msiba huu ni mimi. Marehemu alikuwa rafiki wangu wa dhati tuliyeshirikiana naye sana. Nilimjua marehemu tukifanya kazi katika soko la Mauzoduni na tangu siku hiyo tumeishi kama ndugu; kuomba radhi ukikosewa; kusaidiana, na kadhalika.
Habari za kifo chake zilinipiga kwa mughdha. Sikuamini kwamba amekufa; kwamba sitamwona tena aushini mwangu. Ninasikitika sana lakini kwa kuwa Mungu hakosi, ninaamini kwamba alimpenda zaidi ya tulivyompenda. Ombi langu kwa Mungu ni moja, kwamba amweke rafiki yangu mahali pema peponi; au popote alipojitafutia siku zake za uhai; nami nitakapokufa anipeleke papo hapo tuendelee kuwa marafiki. Mwenzangu lala. Lala salama tutaonana siku moja"
Sajili ya Michezoni

Lugha ya michezoni hutumiwa wakati wa mashindano ya michezo kama vile kandanda, ukimbiaji n.k Hii inaweza kuwa lugha ya watangazaji/wasimulizi wa mchezo, watazamaji, mashabiki au wachezaji.
Sifa za Lugha ya Michezoni
1.  Hutumia msamiati wa kipekee unaohusu michezo kama vile mpira, goli, mchezaji
2.  Huchanganya ndimi na kuingiza maneno ya lugha nyingine kama vile Kiingereza. mfano 'goal!!!'
3.  Ni lugha ambayo hutumia vihisishi na mshangao kwa wingi
4.  Sentensi nyingi katika lugha hii huachwa bila kukamilika hasa hali inapobadilika uwanjani
5.  Husimuliwa kwa haraka haraka ili kuambatana na kasi ya mchezo
6.  Ni lugha yenye sifa na na chuku kwa mfano msimulizi anaposimulia sifa za mchezaji fulani
7.  Hutumia misimu kama vile 'wametoka sare'
8.  Hutumia kwa ya kulinganisha ili kuelezea matokeo ya mechi k.m 'walitoka mbili kwa nunge'
9.  Ni lugha yenye kukariri (kurudia rudia) hasa mchezaji anapoumiliki mpira kwa muda mrefu au mwanariadha fulani anapoelekea kushinda katika mbio.
10.                Huwa na sentensi fupi fupi

Mfano wa Sajili ya Michezoni
Nakwambia ndugu msikilizaji hapa mambo yamechacha kwelikweli. Hawa wachezaji wa Manyuu hawacheki na watu leo. Wameamua kuishambulia timu ya Cheusi bila huruma. Kumbuka kwamba hii ni mara yao ya... Lo! Anauchukua mpira pale, mchezaji nambari tisa... Matiksta. Matiksta, Matiksta na mpira. Anaucharazacharaza pale. Anamwangalia mwenzake. Anaupiga mpira kwa kichwa pale! Lo! Mwenzake anaukosa. Akiushika mpira pale ni mchezaji wa timu ya Cheusi, Romana. Romana, Romana anaelekeza mpira kwenye lango la Manyuu. Anaupiga mpira kwa nguvu! Lo! Hatari sana. Hatari sana katika lango la Manyuu. Hatari! hatari! Goooooooooo ooooh! Wameukosa! Goal keeper ameudaka mpira huo. Pole sana wachezaji wa ... Mlinda lango anaupiga mpira huo kwa hasira. Juu kabisa. Anauchukua pale nambari saba, Saruta. Huyu ni mchezaji machahari sana. Mwaka uliopita, alipewa tuzo la mchezaji bora wa mwaka. Ananyang'anywa na mchezaji mwingine hapa. Wanakabiliana kidogo. Huyu mchezaji anaupiga mpira kwa mguu wa kushoto. Lo! Mpira umekuwa mwingi na ukatoka nje.
Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...
Sajili ya Mitaani

Lugha ya mitaani ni lugha inayozungumzwa na vijana mtaani.
Sifa za Lugha ya Mtaani
1.  Ni lugha legevu isiyozingatia kanuni za kisarufi
2.  Huchanganya ndimi
3.  Hutumia misimu kwa wingi
4.  Hukosa mada maalum

Mfano wa Sajili ya Mtaani
Chali:
Hey, niaje msupaa?
Katosha:
Poa. So, mathee yako alikushow naweza kuja?
Chali:
Ha! Masa hana noma. Si unajua nita...
Katosha:
Chali! Unataka aniletee problem?
Chali:
Mimi ni boy wa maplans. Ngoja nifikirie venye tutamshow
Katosha:
Na by the way, kwani umejipaka mafuta ya manzi. Ama ulikuwa na msichana mgani?
Chali:
Oh! Niliscoop mafuta ya Anita. Si unajua nataka kunukia hmmmm...
Katosha:
Ok. So, umefikiria tumshow nini masa yako? Ama nikona idea poa.
Chali:
Nishow hiyo plot, na by the way, nataka unisaidie kuhusu ile deal yangu na Kaunda. Ile ya siz yangu.
Katosha:
Kwanza tutaplan na huyo siz yako, niwe ndiye nimekuja kuvisit. Mamako atakubali
Chali:
Wow! Idea poa. Utakuwa umekuja kufanya homework. Halafu masa akiishia kwa bed. Homework tutaitupa mbali.
Katosha:
So, utamshow Anita nakuja tufanye homework...
Sajili ya Nyumbani

Hii ni lugha inayotumiwa na watu katika familia. Wanaohusika sana katika mazungumzo ya nyumbani ni mama, baba, watoto, majirani na watu wa ukoo. Maswala yanayorejelewa sana ni yale yanayoiathiri jamii/boma hilo.
Sifa za Sajili ya Nyumbani
Sifa za sajili ya nyumbani hubadilika kulingana na mada inayorejelewa, wanaozungumza na hali katika boma.
Mfano wa sajili ya nyumbani
Baba:
Mama Kadara! Huyo mtoto wako amekuja?
Mama:
Kadara ni mtoto wetu; mimi na wewe.
Baba:
Hapana! Mimi sizai malaya. Huyo ni wako. Hata Bahati ni wako! Hakika wote sita ni wako…
Mama:
Mume wangu unanifanya nikasirike bure tu. Mbona umeanza mafarakano tena.
Baba:
Mafarakano! Mafarakano! Ni mimi niliyekwambia uzae wasichana sita…
Mama:
Lakini sikuzaa pekee. Tulizaa na wewe, mume wangu….
Baba:
Hapana! Uliniona na mimba? Uliniona na maumivu ya uzazi? Umeniona nikinyonyesha mtoto? Mwanamke kuwa na adabu. Nitakurudisha kwa wazazi wakufunze heshima. Na nitaoa sioni tukikaa pamoja.
Mama:
(baada ya kimya) Niambie ulichotaka kuniambia kuhusu Kadara (akijipangusa machozi kwa kitambaa) unajua mume wangu, nakuheshimu. Yangalikuwa mapenzi yangu tungepata wavulana pia. Lakini haya ni mapenzi ya Mungu.
Baba:
Kadara akija umpe kuku apeleke vileoni kwa Mzee Magoti. Nina deni lake kubwa baada ya kunywa tembo siku kadhaa bila kulipa. (akicheka) Hakika hata anastahili mbuzi.
Mama:
Hatuwezi kulipia pombe kwa mbuzi wala kuku. Kuku waliobaki hapa ni wangu na wa watoto wangu. Kuku wako uliwauza.
Baba:
Kelele za chura hazimkatazi ng'ombe kunywa maji. Endelea kupayuka kama wanawake wengine wa kijijini. Nikirudi nikute chakula na maji moto tayari.
Mama:
(akinuna) Haya nimesikia.
Sajili ya Shuleni

Hii ni rejista ya lugha inayopatikana katika mazingira ya shule. Wahusika wake huwa walimu, wazazi na wanafunzi.
Sifa za Sajili ya Shuleni
1.  Matumizi ya istilahi (maneno maalum) yanayopatikana katika mazingira ya shule kama vile darasa, mitihani, vitabu, elimu, muhula, masomo
2.  Lugha yenye heshima kutokana na utofauti baina ya mwanafunzi na mwalimu, mzazi na mwalimu;
3.  Takriri - mbinu ya kurudiarudia maneno. Katika darasa mwalimu hurudia rudia maneno ili kusisitiza anachofunza
4.  Ni lugha yenye maswali mengi na majibu. Mwalimu huuliza maswali wakati wa mafunzo. Wanafunzi pia huuliza maswali ili kujua/kupata ufafanuzi.
5.  Hutumia lugha ya kukosoana na kurekebishana.

a) Mfano wa Mazungumzo katika Sajili ya Shuleni
Mwalimu:
Mzee Kundu, ningetaka tuzungumze kwa muda kuhusu hali ya mwanao, Machome Kundu.
Mzee:
Machome? Ana nini mwanangu.Kuna nafasi imepatikana ya…
Mwalimu:
Mwanako amebadilika sana kitabia. Alikuwa akifanya vizuri sana katika masomo
Mzee:
Kweli kabisa. Mimi ni mlezi mwema sizai watoto mbu mbu mbu darasani.
Mwalimu:
Ndivyo. Lakini sasa naona ameanza kubadilika. Ameanza kulegea katika mitihani na kuzembea kazini.
Mzee:
Unamaanisha nini? (akiinuka) Inaonekana siku hizi hamjui kuwapa adabu watoto. Ni lazima mtoto wangu amepotoshwa na wengine, katika vikundi vibaya!
Mwalimu:
Hakika, mwanako ndiye anayepotosha wanafunzi wengine. Yeye ni kiongozi wa makundi haramu shuleni, yanayovuruga masomo, kuuza dawa za kulevya na mambo kama haya. Hii ndiyo sababu nimekuita tujadiliane. Ni lazima mienendo hii imechipuka nyumbani.
Mzee:
Ajapo nyumbani, mwanangu huzingatia vitabu pekee hata mamake anaweza kuthibitisha haya. Ikiwa kuna utovu wa nidhamu nina hakika haya yanatoka darasani.
Mwalimu:
Tafadhali keti mzee (akichungulia dirishani) Mtindi! Niitie Machome…
b) Mfano wa Mazungumzo katika Sajili ya Darasani

Mwalimu:
Toeni vitabu vyenu vya Historia mnakili haya. Ni nani atakayetukumbusha tulichosoma wiki jana? Naam Halima!
Halima:
Tulisoma kuhusu Chama cha Mapinduzi
Wanafunzi:
(Wakiinua mikono na kupiga kelele) Mwalimu Mwalimu
Mwalimu:
Inueni mikono nitawaona. Msipige kelele. Halima umenoa. Simama! Mwanafunzi mwengine?
Jadaha:
Tulisoma kuhusu kundi asi la Maji Moto lililopinga wakoloni.
Wanafunzi:
Mwalimu! Mwalimu! Kundi la Maji Maji.
Mwalimu:
Naam mmepata. Lakini nimewaambia msijibu kwa pamoja. Ukitaka kujibu uinue mikono. Jadaha, ni kundi la Maji Maji siyo Maji Moto. Leo tutasoma athari za kundi katika taifa letu la Tanzania na namna lilivyoshindwa nguvu. Lakini kabla hatujaendelea ningependa mniambie, ni matatizo yepi yaliyochochea kuchipuka kwa kundi hilo.
Kirata:
Mwalimu nina swali. Kiongozi wa kundi hilo alikuwa nani?
Mwalimu:
Kirata hukuwa darasani wiki jana. Nione baada ya kipindi hiki. (wanafunzi wakicheka) Nawe wafanyani na kitabu cha Hisabati katika somo la Historia. Kimbia ofisini uniletee kiboko. Ninyi ndio mnaorejesha nyuma darasa langu katika mitihani.
Sajili ya Simu

Hii ni lugha inayotumiwa katika mazungumzo ya simu.
Sifa za lugha ya simu
1.  Mazungumzo ya simu ni mafupi, hutumia sentensi fupi zenye muundo rahisi.
2.  Hoja hutajwa moja kwa moja bila maneno mengi kwani ili kudhibiti gharama ya simu
3.  Huwa na kukatizana kwa maneno kati ya wazugumzaji.
4.  Huwa ni mazungumzo baina ya watu wawili pekee; anayepiga na anayepokea.
5.  Hutumia istilahi maalum za lugha ya simu kama neno 'hello'
6.  Huchanganya ndimi (kutumia maneno yasiyo ya lugha nyinginezo) ili kuwasilisha ujumbe kwa upesi.
7.  Ni lugha ya kujibizana.

Mfano wa Sajili ya Simu
Sera:
Hello. Ningependa kuongea na Mika.
Sauti:
Subiri kidogo nimpatie simu.
Sera:
Hello
Mika:
Hello. Sema Sera. Niko kwa mkutano…
Sera:
Pole kwa kukusumbua. Unakumbuka safari yetu ya kesho?
Mika:
Siwezi kusahau. Tunakutana saa ngapi?
Sera:
nampendekeza saa tano machana…
Mika:
Katika Hoteli ya Katata Maa
Sera:
enhe. Hapo kwa heri
Mika:
Haya. Bye!
Maswali.
a)ainisha matawi ya isimu
1.Isimu saikolojia 2.Isimu falsafa 3.Isimu tumizi 4.Isimu tiba 5.Isimu Tiba 6.Isimu Fafanuzi 7.Isimu Jamii 8.Isimu Historia
b)ni nini maana ya fonolojia   sintaksia   mofolojia  semantiki
Fonolojia ni tawi la sayansi ya isimu. Inashughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Matokeo ya uchunguzi wa kifonolojia yana umuhimu katika kubuni alfabeti. Dhana ya fonolojia inajipambanua vizuri zaidi ikifasiliwa kwa kutofautishwa na fonetiki. Wakati fonetiki ni taaluma inayochunguza sauti zitamkwazo na binadamu bila kuzihusisha na lugha yoyote, fonolojia huchunguza mfumo wa sauti wa lugha mahususi kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kimwera, na Kinyaturu. ZINGATIA: Fonetiki huchunguza sauti zote zitamkwazo na binadamu; fonolojia huchunguza MFUMO WA SAUTI wa lugha mahususi.
sintaksia ni aina ya sarufi inayojishughulisha na muundo wa maneno katika sentensi.pia hii tawi huhusika uchnganuzi wa aina za maneno,vipashio vya tungo pamoja na aina zake.
semantiki ni tawi la isimu linalojihusisha na uchunguzi na upambanuzi wa maana.ambapo maana inapambanuliwa na kupewa maana kamili au ya msingi. ingawa na maana za ziada huwepo. mfano, neno mama. maana yake ya msingi kabisa ni mzazi wa kike. wakati maana za ziada ni kama vile mtu yeyote ambaye ni mlezi wa familia,pia kama mke wa mtu.
MASWALI
.
a)Fafanua dhana hizi(alama 3)
i)Lafudhi
ii)Krioli
iii)Lahaja

b)Hujambo: You look familiar Nilikuona wapi my friend?
i)Mtindo huu wa kutumia lugha unaitwaje? Eleza (alama 2)
ii)Eleza sababu tatu kutumia mtindo huu wa lugha(alama 3)
iii)Pendekeza njia tatu za kuondoa mtindo huu wa lugha(alama 3)

c)  Taja na ueleze sifa tano za lugha ya michezoni (alama 10)

Tuesday, 26 July 2016

Dhamira katika mashairi ya Kahigi na mulokozi

DHAMIRA KATIKA MASHAIRI YA KAHIGA NA MULOKOZI

 K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi: Malenga wa Bara
Kitangulizi
Majina ya K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi si mageni katika uwanja wa iasihi ya Kiswahili. Kati ya kazi zao mbalimbali zilizokwishachapishwa za Mashairi ya Kisasa. (TPH, 1973) Malenga wa Bara (EALB, 1976) na Kunga za Ushairi na Diwani Yetu (TPH. 1982) ndizo ambazo zimewapa nafasi muhimu katika dunia ya ushairi wa Kiswahili. Pamoja na hizo, MuIokozi pia amechapisha tamthilia ya kihistoria inayotumia mawanda ya kiepiki kueleleza maisha ya shujaa Mkwawa, Mukwawa wa Uhehe (EAPH, 1979) naye Kahigi akishirikiana na R.A. Ngemera wamechapisha tamthilia ya Mwanzo wa Tufani (TPH, 1977) yenye kuchambua masuala mabalimbali ya kitabaka katika jamii. Katika kazi zote hizi waandishi hawa wanashughulikia dhamira kadhaa zinazohusu nyanja za utamaduni, saisa na uchumi katika maisha ya Watanzania na Waafrika kwa jumla.
DHAMIRA KUU
Katika diwani yao ya Malenga wa Bara, washairi wamekabili dhamira mbalimbali, hasa za:
1. Maana ya uhuru
2. Dini na kifo, pamoja na maana ya maisha
3. Kumtetea mkulima na mtu mnyonge
4. Matumizi ya nguvu kama njia ya ukombozi wa wanyonge
5. Mjadala kuhusu masuala ya utamaduni
6. Uzalendo na Wasifu
7. Mapenzi
8. Namna tunavyoishi.
Maana ya Uhuru
Mashairi kadhaa yanachunguza maana ya uhuru. Katika shairi la kwanza la "Vuteni Makasia," kwa mfano, washairi wanatumia taswira ya safari kuonyesha kuwa harakati za kutafuta uhuru ni sawa na safari ndefu baharini yenye matatizo mengi (kupigwa risasi, mbundu za adui, vifo, n. k.).
Tunawaona wavuta makasia (wapigania uhuru) wakifurahia ushindi baada ya kunusurika na vishindo vya adui:
10. Wakapiga yowe wakifurahika

"Hakika kweli sasa tumeokoka",

11. Na kila mmoja akafikiria

Vipi mke wake atampokea.
Katika shamrashamra hizi za ushangiliaji, wavuta makasia hawa wanasahau kuwa mwisho wa safari bado. Hii ni tahadhari inayotolewa kuhusu maana ya uhuru; kuwa uhuru si lelemama, ni mapambano ya kuulinda na kuutetea uhuru huo pamoja na kuupalilia. Ushindi tuuonao mwanzoni mwa shairi ni ishara tu ya uhuru wa bendera na wa wimbo wa taifa. Uhuru huu si kamili kama ule wa kiuchumi na kiutamaduni haujapatikana. Kuangamia kwa wavuta makasia mwishoni mwa shairi ni ishara ya kuangamia kwa taifa ambalo baada ya kupata uhuru wa mwanzo lilijisahau likaendelea tu kuusherehekea uhuru huo, bila kuujengea misingi imara ya uchumi, utamaduni na itikadi sahihi.
Shairi la "Kitu cha Kutamani" (uk. 4), pia linaongelea faida za uhuru kwa kutueleza juu ya "uhondo" na "tulizo". Hata hivyo washairi wanasisitiza kuwa mtu apatapo uhuru hana budi kuulinda:
Ni kitu cha kutamani
Cha lazima kwa insani
.....................................
Uhuru ukiupata
Ulinde kwayako mata
Ubeti wa mwisho wa shairi hili nao hali kadhalika unasisitiza jambo hili kwa kueleza kuwa uhuru sio mwisho wa harakati. Hili limekaziwa pia katika shairi la "Uhuru" (uk. 14) ambalo limesisitiza kuwa uhuru si kula makombo hata kama makombo hayo yawe yamenona kiasi gani. Kwa vile shairi hili ni muhimu na fupi tutalidondoa lote:
1. Ni heri kula karanga, na matunda yenye koko,
Na mapumbaya kusaga, yenye wingi wa mnuko,
Kuiiko kuta kumwaga, uhondo mchanganylko,

Na holi uhuru wako, umekwisha kuuaga.

2. Ni heri kutangatanga, kama moshl wa tambiko,
Bila nyumba yo kujenga, bila sikani la kwako,
Kuliko kuwa na uga, na majumba na majiko,

Na hali uhuru wako, umekwisha kuuaga.

3. Ni heri kuyuga yuga, kwa wele na sekeneko
Kuoza kama uyoga, kufunikwa maumboko
Kuliko kuzidi ninga, uzuri wa mwili wako
Na hali uhwu wako, umekwisha kuuaga.
Katika beti hizi tatu washairi wanaeleza juu ya umuhimu wa mtu kujitegemea badala ya kutegemea mikopo na "sadaka" zenye kuhatarisha uhuru wake. Kwa hiyo basi, ni vizuri nchi zijaribu kujitegemea hata kama ni masikini kuliko kuishi maisha ya kuwa na wafadhili wa nje ambao katika kujidai "kusaidia" hapo hapo huwa wanazibana nchi hizo ziuze uhuru wao.
Taswira ya safari imerudiwa katika shairi la "Kwenye Safari Barabarani" (uk. 37) kusisitiza maana ya uhuru ilivyoshikamana na harakati. Hapa kauli ya "Uhuru ni Kazi" inajidhihirisha, na ubeti wa mwisho unauona uhuru kama "gogo zito" ambalo linahitaji tahadhari wakati wa kulisukuma. Umuhimu wa tahadhari hii umejitokeza tena katika shairi la "Mchumba Wangu" (uk. 91). Uhuru hapa ume-fananishwa na mchumba ambaye bila kuchukuliwa kwa uangalifu huweza kumgeuka huyo mwenye mchumba pa kumwangamiza. Beti za 9 na 11 zinaoayesha jambo hili:
9. Hizo pesaze akanza kunihini,
Na kunipokonya zangu kwa uhuni,
Kitwaa kizituma kwao nyumbani,

Sikuweza kuamini!
11. Na nilipotaka kumpa talaka,
Aliita majitu yakanitandika,
Nikapigwa kweli hata nikanyoka,

Sasa siwezi kuwika.
Beti hizi zinaonyesha nguvu za ukoloni mambo-leo, hasa pale ambapo nchi iliyopata uhuru wa bendera imenaswa na mtego wa ulaghai wa mataifa ya kibepari. Kupoteza uwezo wa "kuwika" ni ishara ya kupokonywa uhuru wa kujiamulia mambo. Katika ubeti wa mwisho mshairi anashauriwa kuwa ili kurekebisha yote hayo nguvu hazina budi kutumiwa:
14. Ndipo hasubiri siku ya lipizi,
Nitetane na yeye huyu jambazi,
Nimtie risasi ya kimapinduzi,
Nikomeshe huu wizi.
Suala hili la matumizi ya nguvu na umwagaji damu tutalipa nafasi yake ya pekee kwani limezishughulisha sana kalamu za washairi hawa.
Dini, Kifo na Maana ya Maisha
Washairi hawa hawaamini kuwa dini au hata Mungu ana nafasi yoyote muhimu katika maendeleo ya jamii. Kwa hiyo, mashairi yao yote yanayoongelea dini, kifo na Mungu yanakejeli na kutufanya tukidharau kifo, na tusimtegemee Mungu bali tujitegemee wenyewe katika kuleta maendeleo yetu.
Mashairi ya "Tazama Huyo Kipusa" (uk. 6), "Nikifa" (uk. 7), "Saa ya Mwisho" (uk.10), "Hatima ya Kila Mwali" (uk.22), "Baada ya Matanga" (uk.42), na "Dawa Mbili" (uk.54) ni mifano ya yale yashughulikiayo kifo kwa kuonyesha kuwa kufa ni jambo la kawaida, na kwamba hakuna haja ya kusikitishwa sana nacho.Katika mashairi hayo washairi wameonyesha pia kwamba maisha ni jambo ambalo kama lilivyo na mwanzo, lazima liwe na mwisho pia. Msichana mzuri tumwonae katika "Tazama Huyo Kipusa" na "Hatima ya Kila Mwali" twamona mwishowe akiwa kazeeka na sura yake nzuri ikiwa imechujuka. Taswira hii imetumiwa katika kuonyesha hatima ya maisha ya mwanadamu.
Kwa washairi hawa kifo ni mwisho wa maisha, na hakuna tena maisha ya ahera walajehanamu kwani, kama wasemavyo: "Kumbukizi la mkasa, ni rutuba kuipata."
Washairi hawa wanapopinga udhanifu uliopo katika dini na imani zilizoegemea kwenye nguvu zilizo nje ya uwezo wa mtu na mazingira yake, hapo hapo wanamtahadharisha mtu mnyonge, hasa mkulima, kuwa asiamini kwamba unyonge wake pamoja na shida anazokabiliana nazo hutokana na mambo yaliyoko nje ya uwezo wake. Jambo hili linachangia katika dhamira ya utetezi wa mtu mnyonge, hususan mkulima; dhamira inayofuatia karika mjadala wetu.
Kumtetea Mkulima na Mtu Mnyonge
Mashairi ya "Maombolezo ya Mtu Maskini" (uk.15), "Siku Itafika" (uk.21), "Kauli ya Madhulumu" (uk.33), "Ngonjera" (uk.43), "Vilio vya Dhiki" (uk.53), "Ni Rahisi Kula Kuliko Kulima" (uk.62) "Mwangalie Mkulima" (uk.67), "Kilio Kisikikapo" (uk.69), "Sima na Mayai" (uk.70). "Siku Yetu" (uk.90), "Mimba na Zao Lake Usizaliwe" (uk.94), "Nilipozaliwa" (uk.95), na "Nyimbo za Kijiji" ni baadhi ya mifano ya mashairi yanayojihusisha na dhamira ya kumtetea mkulima na mtu mnyonge. Kwa vile haya ni mengi sana katika diwani hii tutachukua machache kuwa vielelezo.
Shairi la "Maombolezo ya Mtu Maskini" limetumia tamathali nzito nzito kuonyesha undani wa dhiki za masikini. Linaongelea "panya wa uhitaji", "simba wa ubepari", "radi ya maradhi", "mishale ya upofu", "shubiri ya ufakiri", "miiba ya dhuluma" na "funza wa shutuma". Yote haya yamemwandama mtu masikini. Mtu kama huyu, azaliwapo huwa tayari amekwishaanza kufa. Anaona kuwa haishi bali yupo tu "kama kitu tu, kama kijiwe tu, kama kijitu tu." Lakmi hata hivyo washairi hawamkatishi tamaa mtu huyu kwani, kama wasemavyo:
Siku ya wokovu ipo,
Siku ya kukombolewa inakuja!
......................................
Mtu atakuwa mtu
......................................
Na mwanadamu atakuwa huru
Siku hiyo itakapofika mtu mnyonge ataacha "kuwapo na kuanza kuishi." Lakini, ili ukombozi huu upatikane, harakati lazima ziwepo kwani siku hiyo ni ya "kitimbanga kuanguka na chamchela kucharuka." Suala hili la mbinu za wokovu wa mtu huyo mnyonge tutalipatia nafasi ya pekee katika mjadala wetu kwani nalo pia limewashughulisha sana Kahigi na Mulokozi.
Katika "Ngonjera", Mulokozi ameshughulikia mgogoro wa maisha ya mtu mnyonge na kuyatolea suluhisho. Misingi ya suluhisho hili ni zao la athari za Azimio la Arusha, ndiyo sababu linaishia na wito wa kurudi kijijini:

KIJANA:
Sasa sitasitasila


Nitakwenda kwa haraka, furaha kuitafuta,


Kisimanimwa baraka, shamba kulikotakata!
Ijapokuwa kwa nyakati hizi suluhisho hili la kuwarudisha vijijini watu walioshindwa na maisha mjini ni jawabu linaloonekana kupwaya, katika miaka ya mwisho ya sitini na ya mwanzo ya sabini lilikuwa na misingi kwani nguvu za Azimio la Arusha bado zilikuwa na vuguvugu kubwa, na imani za watu katika vijiji, hasa vijiji vya ujamaa, bado zilikuwa juu sana.
Shairi la "Mwangalie Mkulima" linatoa taswira ya hali duni mno ya mkulima ambaye, twaelezwa, katika jitihada zake za kupasua "udongo na miamba", mwishowe unaambulia kibaba tu. Taswira hii imewekwa sambamba na za watu wengine kama vile "kiongozi na tumbole", "Singh na jiduka lake" oa "mtoto rijale" mwenye benzi ambalo hakulitaabikia. Kwa hiyo upande mmoja wako hao wenye vyao, na upande mwingine yuko mkulima na kuli wenye kutiririsha jasho kuwashibisha hao wa kundi la kwanza. Ubeti wa mwisho wa shairi hili unaungana na mashairi yahusuyo uhuru ambayo tumeyaangalia:
7. Naam watawme wote na kisha,
Tafiti tena ramaniya maisha:
Shangwe za uhuru sasa zimekwisha,

Kilichosalia kejeli komesha!
Kejeli wanayotaja washairi hapa ni kuwa badala ya uhuru kuleta usawa baina ya watu katika jamii, utabaka umeendelea na masikini wamezidi kufukarika wakati matajiri nao wameendelea kutajirika. Jambo hili limesisitizwa pia katika shairi la "Sima na Mayai" ambalo linaonyesha jinsi ambavyo hali ya mkulima mwenye kutoa mchango mkubwa katika elimu ya vijana imebaki kuwa duni wakati ambapo hali za wasomi hao zimebadilika na kuwa nzuri. Maisha ya raha na starehe tuyaonayo katika beti za 1, 3, 5, 7, 9 na 11 yanaashiria ukuta uliopo baina ya waliobahatika kupata elimu ambayo imekuwa daraja la kuwavusha hadi ng'ambo ya pili yenye uhondo wa kiuchumi; na yale ya beti za 2, 4, 6, 8, 10, 12, 13, 14, 15 na 16 ambayo ni ya umasikini hohehahe. Hapa basi, dhamira ya elimu na nafasi yake katika jamii inajidhihirisha: elimu hiyo bado haijawa chombo cha wokovu wa wanyonge.
Beti za 15, 16 na 17 zenye kuonyesha uzee na ubovu wa mwili wa mkulima hapo hapo zinaasa kuwa kuna haja kama si kumlipa mkulima kwa kujitolea kwake muhanga katika kuwaelimisha vijana, walau asiachwe
Kufia kando ya njia
Kama mwanamke mgumba
Kama kokwa lisilo na mbegu
Mkulima anayechangia sana katika kulielimisha taifa ni sawa na "mgomba wenye mkungu bora", mgomba ambao hauna budi kuwekewa mhimili ili ujiegemeze juu yake. Huu ni wito wa kuwalipa wakulima kwa elimu waliyopatia jamii.
Hali duni ya maisha ya mkulima imesawiriwa pia katika "Nyimbo za Kijiji "ambazo zinaonyesha jinsi mvua zilivyochelewa na vile ambavyo "mtama umemalizwa na ndege." Hata hivyo, shairi la "Weka Jembe Mpini" linaleta matumaini mema katikati ya dhiki za mkulima ijapokuwa hatuonyeshwi hasa namna mabadiliko yaonekanayo yanavyopatikana.
Matumizi ya Nguvu kama Njia ya Wokovu wa Wanyonge
Suala la utatuzi wa migogoro inayoshughulikiwa na wasanii katika kazi za fasihi lina nafasi muhimu sana wakati wa kuchambua kazi hizo. Wakati ambapo akina Kahigi na Mulokozi wamejihusisha sana na migogoro ya kijamii, na hata kushauri kuwa baadhi yake huweza kutatuliwa kwa kuthamini na kuendeleza kilimo, washairi hawa wanaelekea kusisitiza kuwa NGUVU na kumwaga damu ni lazima ili kuleta wokovu wa mtu mnyonge. Kwa hiyo basi, tunakutana na mashairi kadhaa yanayosisitiza jambo hili katika Malenga wa Bara. Mathalani, katika shairi la "Siku Itafika" (uk.21), washairi wanatuambia:
4. Siku hiyo itafika, itafika, itafika,
Vilio vitasikika, beberu asononeka,
Damu zitatiririka, dhalimu kuhasirika...
Ili "siku hiyo" ya wokovu wa wanyonge ifike, washairi wanatoa wito katika shairi lao la "Njiaya Damu" (uk.32):
Wito unaita: "Shikeni mikuki
Mapanga na miundu na bunduki
Mwende kwenye kituo cha uhaki"
Kwa hiyo basi, kwa Kahigi na Mulokozi haki itapatikana kwa kupitia mtutu wa bunduki, ndiyo maana wanasisitiza katika shairi hilo hilo:
Ninaona bahari kubwa ya damu
Bali najua kutoka kwenye damu
Patazuka maisha mastakimu
Itashere'ka ya uhuru mizimu.
Mkabala huu wa kuuona umwagaji damu kuwa ndilo jawabu la kuleta haki na usawa baina ya watu unajitokeza katika mashairi ya "Mtokoto" (uk.35), "ViliovyaDhiki" (uk.53), "Inuka" (uk.55), "Siku za Bunduki" (uk.56), "Ni Rahisi Kula Kuliko Kulima" (uk.63), "Fundo Kusukasuka" (uk.65). "Siku Yetu" (uk.91), "Mchumba Wangu" (uk.93), "Nilipozaliwa" (uk.96), "Namna Tunavyoishi" (kurasa za 105 · 108) na "Zama Hizi" (hasa ukurasa wa 115). Mashairi mengine ni "Namna Tunavyoishi" na "Zama Hizi" ambayo tutayachambua kipekee baadaye.
Kwa baadhi kubwa ya wasomaji, inawezekana kuwa ushairi wa umuhimu wa utumiaji nguvu na umwagaji damu katika kuleta wokovu wa wanyonge utaonekana kuwa wa kijaziba mno (amachist); na kubakia kuwa ni umwagaji damu kwa ajili tu ya umwagaji damu. Hata hivyo kuna mistari miwili ya mashairi mawili tofauti ambayo inaonyesha dhahiri kuwa siyo nia ya washairi kuuchukulia umwagaji damu kijuujuu tu. Mstari wa kwanza wa "Nipe Mwongozo" (uk.93) unasema: "Nipe mwongozo haraka, na kikoba cha baruti."
Kwa hiyo siyo suala la baruti na bunduki tu bali lazima harakati hizo ziwe na mwongozo kamili. Jambo hili limerudiwa katika mstari wa mwisho wa shairi la "Maombolezo ya Mtu Maskini" ambamo twaelezwa kuwa siku itakapowadia ya "kitimbanga kuanguka" ili mtu mnyonge aache kuwapo na aanze kuishi, hapo ndipo:
Kila mtu ataishi
Na bunduki begani, jembe mkononi
Na kitabu mfukoni.
Kwa kututolea vitu hivyo vitatu: bunduki, jembe na kitabu, washairi wanadhihirisha kuwa matumizi ya nguvu kama njia ya ukombozi wa mtu mnyonge hayana budi kuambatana na ufanyaji kazi pamoja na kuwa na mwongozo kamili.
Hata hivyo, maswali kadhaa yanazuka kuhusu dhamira hii. Je, matunuzi hayo ni dhidi ya nani hasa katika jamii kama ya Tanzania? Nani watashika hizo bunduki? Chini ya uongozi wa nani? Watazitoa wapi?
Mjadala Kuhusu Masuala ya Utamaduni
Kuanzia miaka ya sitini na tano hadi katikati ya miaka ya sabini kulikuwa na vuguvugu la kiutamaduni katika nchi za Afrika. Hii ilikuwa miaka ya Waafrika kujizatiti na hata kuusisitiza Uafrika wao baada ya mkoloni kuondoka. Mawazo ya kusisitiza Uafrika (Negritude) yalipata msisitizo mpya, na hata kwa upande wa siasa itikadi mbalimbali zilianza kutafutiwa misingi ya Uafrika: kukazuka "usoshalisti wa Kiafrika", "Ujamaa; nakadhalika.
Kwa upande wa masuala ya utamaduni katika Afrika ya Mashariki, mjadala ulioanzishwa na Okot pBitek katika utungo mrefu wa Wimbo waLawino (EAPH, 1975) ulisambaa haraka mno mithili ya moto katika mbuga kavu. Cheche za moto huu za kuutetea utamaduni wa Mwafrika zimejitokeza hapa na pale katika diwani hii ya Malenga wa Bara.
Shairi la "Kwa Shaaban Robert" (uk.5) ambalo ni la kitawasifu, papo hapo linatukuza lugha ya Kiswahili, na lile la "Zuka" (uk. 7) linatoa wito wa kufufua utamaduni wa Mwafrika:
Zuka uwke mzuka,
Utamaduni Afrika!
Yule aliyekuteka
Hatarudi kukuteka!
................................
Zuka, Utathaminika

Zuka, utakumbatika.
Katika kusisitiza umuhimu wa kujirudishia hadhi kwa Mwafrika, washairi wanasisitiza-pia umuhimu wa kuchuja katika ujenzi wa utamaduni mpya:
Chuja, uchuje, mchuja
Utamaduni wa tija
Kumbata ule wa haja
Usikumbate vioja;
Kasumba inayofuja,
Hamna haja kuonja!
Kasumba wanazozipinga washairi hapa ni zile zile anazozikemea Lawino anapomshauri mume wake arudie utamaduni wao badala ya kukumbatia kikasumba tamaduni za nje.
Shairi la "Kitu Nisichokitaka" (uk.10) nalo linawekea mkazo umuhimu wa mtu kuwa na uasili katika utamaduni wake badala ya kuvaa tamaduni za nje zenye kumfanya aooekane kama mwenye nguo iliyojaaviraka. Shairi la "Wimbo Uliosahaulika" (uk.87) haU kadhalika linasuta kuabudu mambo ya nje: kuanzia "mitishamba ya kigeni inayoukwajua mwili wangu" - hapa ikamaanisha madawa ya kigeni kama vile Ambi wanayotumia baadhi ya Waafrika ili kujaribu kuiondoa "aibu" ya weusi wa ngozi zao na kuwafanya wawe weupe kama Wazungu - pamoja na "utumwa (wa) talasimu za kigeni shingoni.../na mizimu nisiyoijua...," mambo ambayo yanaashiria dini na imani ngeni zinazomfanya Mwafrika awe mtumwa wa mawazo nchini mwake. Beti za 4, 5, 6 na 7 za shairi hili zinatoa uamuzi wa hatua za kuchukuliwa katika kurudia utamaduni wa Mwafrika na kutupilia mbali kujidharau.
Japokuwa dhamira kuu katika shairi la "Mlima wa Kimombo" (uk.97) ni ile ihusuyo aina ya elimu itolewayo katika jamii, washairi pia wameihusisha dhamira hiyo na masuala ya utamaduni, kwani katika elimu hii kuna kuvaa "pekosi kike, Nywele za wafu, Kucha za damu." Haya ndiyo yale yale anayoyapiga vita Lawino dhidi ya akina "Klementina'' wa Afrika.
Kwa jumla tunaweza kusema kuwa mashairi yote ambayo yamejishughulisha na masuala ya utamaduni katika diwani hii, hapohapo yameungana na yale yaelezayo maana ya uhuru kwani sehemu mojawapo muhimu ya uhuru wa mtu inahusu kuthamini na kuuamini utamaduni wake.
Uzalendo na Wasifu
Uzalendo ni mapenzi ya mtu kwa nchi yake; ni kipimo cha yale mapenzi aliyo nayo mtu kwa wanajamii wenzake. Kwa maana hiyo ya harakaharaka basi, itadhihirika wazi kuwa "uzalendo" wauonyeshao Kahigi na Mulokozi katika diwani ya Malenga wa Bara umepevuka zaidi ya ule wa Mashairi ya Kisasa uliokuwa wa kuisifu tu nchi katika ukubwa wake: mapenzi yasiyo na welekeo wowote (angalia kwa mfano mashairi ya "Nitaisifu Tanzania" na "Nakuahidi Tanzania")
Mashairi ya "Kwa Shaaban Robert" (uk.5) "Sudi ya Tanzania" (uk.36), "Nchi Yangu Utadiriki" (uk.80) na "Kiswahili" (uk.84), ni ya wasifu na kizalendo, na hapohapo yanamtetea mtu mnyonge. Haya yanaungana na yale ya kumtetea mkulima na masikini, na kudhihirisha kwamba dhana ya uzalendo ni suala la kitabaka. Mtu hawezi kuipenda nchi tu katika ukubwa wake bila kuelekeza hisia zake za mapenzi kwa tabaka fulani katika nchi hiyo. Kwa mfano, katika shairi la "Nchi Yangu Utadiriki", zaidi ya kuonyesha mapenzi yao kwa Tanzania, hapohapo washairi wanasisitiza kuhusu mapinduzi yatakayowainua makabwela baada ya kuzinduka na kutambua uhalisi wa utabaka wa jamii katika ubeti wa mwisho:
Tanzania utadiriki
Kwa taayo ya mapinduzi,
.......................................
Watazinduka makabwela,
Watainuka makabwela,

Zitakatweni silisila!
Uzalendo wa akina Kahigi na Mulokozi, basi, si ule wa kuipenda nchi kwa ajili ya kuipenda tu, bali umeelekezwa kwa tabaka la wanyonge kama vile makabwela.
Mapenzi
Robo nzima ya kitabu cha Mashairi ya Kisasa ni ya mashairi ya mapenzi baina ya wavulana na wasichana; mapenzi ya "sili silali". Ijapokuwa hapa na pale ile hali ya "sili silali" inaibuka katika Malenga wa Bara, washairi wamepunguza sana idadi ya mashairi ya mapenzi ya namna hiyo. Wakati ambapo mashairi ya "Barua Kwa..." (uk.39), "Wimbo Kabla ya Kulala" (uk.79), na "Mapenzi" ni ya kuonyesha tu hisia za mtu kwa mpenzi wake, yale ya "Sifa Zako Nitataja" (uk.24) na "Asali ya Nyuki" (uk.83) japokuwa ni ya mapenzi pia, yanatoa ujumbe wenye kupevuka zaidi ya ule wa "sili silali". Kwa mfano katika "Sifa Zako Nitataja", baada ya sifa mzo mzo ambazo zimetolewa kuhusu mpenzi mwenye umbo na sura nzuri sana, tunajulishwa kuwa jina la mpenzi huyo ni Kapesa. Jina hili linatupa maana nyingine ya shairi hili ambayo inaungana na ile ya dhamira ya fedha inavyoabudiwa katika jamii.
Namna Tunavyoishi
Yako mashairi mawili katika Malenga wa Bara ambayo ni muhimu sana kwani yanatoa taswira ya maisha yalivyo katika jamii yetu nyakati hizi. Hayo ni "Namna Tunavyoishi" (uk. 105) na "Zama Hizi" (uk. 113). Kwa vile haya yana umuhimu wake, uchambuzi tutakaofanya wa mashairi haya, hasa wa lile la "Namna Tunavyoishi", utafuata ubeti hadi ubeti; au walau utazingatia mafungu ya beti zenye kushirikiana.
Beti mbili za kwanza za shairi la "Namna Tunavyoishi" zinauliza maana ya uhuru na pia maana ya maisha hasa pale ambapo "uhuru" na maisha hayo yamezungukwa na taabu, vilio, afya mbaya, na watu ambao hawaishi bali wanadumu tu. Taswira hii ya dhiki imesisitizwa katika beti za tatu na nne ambazo zinaeleza jinsi maradhi mbalimbali yalivyoenea katika jamii. Beti za tano hadi kumi na moja zinaonyesha kuwa badala ya kukaa na kulalamikia dhiki, watu wanyonge hawana budi kuharakatika. Washairi wanaziona harakati hizi kuwa sawa na safari juu ya barabara iliyo na kokoto. Wanasema:
Na katika kupigana, hutokea tukakonda
Ya kokoto kalisana, barabara ina nunda
Lakini wanasisitiza kuwa kwa vile umma wa watu hauwezi kukaa tu na kuvumilia dhiki ziletwazo na "zimwi na vifutu" (viongozi wapotofu), basi nguvu lazima itumiwe ili kuleta mabadiliko yanayotakiwa, kwani, kama wasemavyo wenyewe:
Maisha ni harakati, mazingira kuyadhidi
Hajaya kunyonya titi, la uhai kufaidi
Na mtu kila wakati, budi awekejuhudi
Lau kwenye harakati, atashindwa na hashindi.
Katika kuyaangalia maisha ya leo, washairi wameonyesha uzuri na ubaya wa maisha hayo; lakini wamesisitiza ile dhamira ambayo imewashughulisha sana katika ushairi wao: kwamba uhuru si sherehe zisizo na mwisho. Maisha ya leo hayajatufikisha mahali pa kusherehekea:
Haujajiri wakati, wa mtu kushereheka
Akalinyonya na titi, kwa raha kufaidika
Kilasiku harakati, zinazidi kucharuka
Kinyume na E. Kezilahabi katika diwani yake ya Kichomi (Heinemann, 1974) ambamo mashairi yake mengi yanakatisha tamaa, Kahigi na Mulokozi katika Malenga wa Bara, na hasa katika shairi hili la "Namna Tunavyoishi", wamesisitiza kuwa ushindi wa watu wanyonge hauna budi kupatikana kwani lazima "kule mbele kupateka."
Kwa Kahigi na Mulokozi, dunia ya leo imezungukwa na uovu na uozo mwingi sana ambao lazima upigwe vita japokuwa baadhi ya mafundisho ya dini hudai kuwa mabaya yote yatalipizwa siku ya kiyama. Wanasema:
Japo Dini zimezuwa, etimoto utazima
Bali sisi tunajuwa, kuwa hakuna kiyama
Mwanga wa moto muruwa, hakuna wa kuuzima.
Kwa washairi hawa, zama zetu bado si za uhuru kamili, ndiyo maana shairi linamalizia na wito wa kusimama imara kuuwania uhuru ili kuangamiza dhiki na kuleta "ngoma mpya ya dunia."
Maudhui ya shairi la "Zama Hizi" yanalandana sana na ya shairi la "Namna Tunavyoishi". Shairi linasisitiza kuwa dhiki zimekithiri, magonjwa yamesambaa, na uhuru si uhuru kamwe: hata ule "uhuru" uliopatikana mwanzo umetekwa nyara huku wale walioshiriki katika kuupigania wanaendelea na maisha duni:
Sasa asaliya Uhuru yaliwa na kiboko wa inda,
Na mashujaa wajana walamba midomo mikavu
Kote kuna vilio vya nyasi na miti inayoungua
Dhamire Nyinginezo
Katika kuchambua dhamira mbalimbali zinazojitokeza katika Malenga wa Bara tumeorodhesha mashairi kadhaa kwa kila dhamira. Mashairi hayo yanawakilisha tu orodha ndefu zaidi, na ni juu ya msomaji kuyaangalia yale ambayo hayajaorodheshwa na kujaribu kuyachambua na kuyaainisha.
Hata hivyo, hapa tutaangalia baadhi ya mashairi mengineyo ambayo kidhamira yanajitegemea.
Shairi la "Jua la Dhahabu" (uk.18) linaongelea Azimio la Arusha na jinsi ambavyo, sawa na jua,
Miali yake imepenya
Anga la nchi yangu
Na kukifukuw kiw
Kiza kinachoongelewa hapa ni ubepari na unyonyaji ambao ulipigwa vita na Azimio la Arusha. Jua hili linatakiwa liwake ili liwamulikie wanyongc vidato vya kupandia kuelekea kwenye neema na maendeleo yatakayowasha tabasamu katika mioyo yao. Nguvu hizi za Azimio zimeelezwa pia katika shairi la "Ngoma ya Radi" (uk.110) ambalo Umeonyesha jinsi ngoma hiyo ilivyowazindua wanyonge.
Kati ya mashairi yote ya diwani hii, shairi ambalo linaonekana limekosa welekeo, halina kichwa wala miguu, ni lile la "Vita" (uk.l9) lenye beti zote ishirini na mbili zikishangilia vita ambavyo hatuelezwi ni vya nani, bali kupewa tu vidokezo vinavyopwaya katika ubeti wa pili na wa tatu vyenye kugusia kuwa vita hivi ni vya watu ambao,
Bezo wamepita
Kwonyesha wataka, kuwasio duni
Kwonyesha hakika, kuwa si manyani
Vidokezo hivi havitoshi kutueleza kwa hakika kama vita hivi ni vya kumpigania nani hasa.
Shairi la "Buyu la Kaya Limevunjika" (uk.29) ni la maombolezo na kilio cha watoto kwa kutokwa na mama yao. "Buyu la kaya" ni ishara ya shibe na uhai, kwani aghalabu buyu hutunzia maziwa ambayo hupendwa sana na watoto. Lakini pia katika shairi hili nafasi, na hata dhana ya mama katika familia imeelezwa. Twaelezwa kuwa wakati mama alipokuwa hai nyumba ilikuwa inang'ara na kunukia. Ila:
Sasa uchafu umetanda, mnuko umechacha

Na haipo furaha,
Shairi hili basi, linaonyesha kuwa nyumba bila mama si nyumba: ni mahame ambamo hamna uhai, furaha wala raha.
Shairi la "Soga" (uk. 85) - shairi ambalo linatumia sana ucheshi katika kuyatoa maudhui yake - linaasa kuwa kila hali na kila kitu kina pande kuu mbili, na kusisitiza dhamira ya nguvu za pesa katika jamii. Washairi wanasema:
Na dunia ni mfuko na nchi zote ni masoko!
Fedha ndiyo bwana, fedha ndiyo Mungu

Anayekanusha hamjui Mungu!
Washairi wameamua kumalizia diwani yao kwa shairi lenye kuleta matumaini kwa wanyonge. Shairi la "Siku Imefika" (uk.120) linaeleza jinsi ukoloni wa Mreno ulivyoangushwa, na jinsi kaburu anavyopapatika kutokana na harakati za ukombozi. Ni shairi la nderemo, chereko-chereko na la kuleta matumaini mema kwa wote wanaonyonywa, wanaonyanyaswa na kuonewa.
MATUMIZI YA BAADHI YA VIPENGELE VYA FANI
Katika kuzichambua dhamira mbalimbali za Malenga wa Bara, kila mara tumekuwa tukigusia pia masuala ya fani. Kwa mfano, katika kuiangalia dhamira ya "Maana ya Uhuru" tulitaja jinsi taswira ya safari ilivyotumika kueleza dhana ya uhuru. Mashairi ya "Vuteni Makasia", "Kwenye Safari Barabarani", "Msafiri Mpya" (uk.40), na "Kauli ya Mzee" (uk. 22) yametumia pia kipengele cha fani cha taswira ya safari kutolea maudhui yake yahusuyo harakati za ukombozi za kujitafutia uhuru kamili. Vipengele vingine vikuu vya fani walivyotumia Kahigi na Mulokozi katika diwani yao ni:
1. Tamathali za semi
2. Misemo, methali na nahau
3. ishara ya ngoma
4. Taswira za usambamba
5. Majigambo
6. Mtindo wa tambo
7. Mtindowavinanamizani.
Tamathali za Semi
Tamathali za semi zimetumiwa katika mashairi mengi humu kutajirisha maudhui, na pia kuleta picha kamili ya lile wanaloiieleza washairi.
Mathalani, katika sbairi la "Vuteni Makasia" tunaelezwa hivi kuhusu mwendo wa mashua:
9. Mashua ikenda ikichachamaa
Uso wa bahari ikiuchubua
Hii ni tashihisi, kwani, kama tujuavyo bahari haina uso uwezao kuchubuliwa, bali uso huu ni wa kuwazika tu.
Shairi la "Maombolezo ya Mtu Masikini" limejazana tamathaii zenye kuonyesha undani wa dhiki za mtu masikini kama vile "panya wa uhitaji", "simba wa ubeberu", "matiti ya uwingu wenye ubahili". Yote haya yamesaidia kueleza vizuri zaidi dhiki hizo kuliko vile ambavyo ingekuwa kama washairi wangetumia maneno kama vile "ubeberu mbaya", "maradhi mengi", na kadhalika, ambayo ni ya kawaida mno.
Katika shairi la "Sima na Mayai" mzazi anamuasa kijana wake kwa njia ya tamadhali asemapo:
16. Usiniache kufw kando ya njia
Kama mwanamke mgumba
Usiniache ning'oke kamo muyombo
Usio na mzizi wa hati
Tamathali ya tashbiha imetumika - hapa kusisitiza umuhimu wa wasomi kuwahudumia wale wahowasomesha. "Mwanamke mgumba." "kokwa lisilo na mbegu" na "muyombo usio na mzizi wa kati" ni ishara za viumbe wasio au visivyo na uwezo wa kuendeleza uhai duniani. Mzazi anayelalamika katika shairi hili wakati huohuo anamdai kijana wake kuwa yeye si nigumba, si kokwa lisilo na mbegu wala si muyombo usio na mzizi wa kati kwani tayari ameshadhihirisha uwezo wake wa kuendeleza maisha kwa kumzaa kijana huyo msomi. Uwezo huo pia tunaweza kuuchukulia kiishara kuwa ni kule kujitolea kwa mzazi au jamii kuwasomesha vijana.
Mfano mwingine wa matumizi ya tamathali umo katika shairi la "Kwa Shaaban Robert" ambako twaelezwa kuwa maandishi yake ya kudumu yanakata "kama panga.''
Ni dhahiri kuwa iko mifano mingi mingine ya tamathalt za semi katika diwani hii ambayo wasomaji huweza kuitafiti na kuigundua wenyewe.
Misemo, Methali na Nahau
Mashairi kadhaa katika diwani hii yametumia misemo, methali na nahau si kama njia ya kupamba tu bali pia katika kutajirisha yale yanayoongelewa.
Mathalani, katika shairi la "Saa ya Mwisho, (uk. 10) msemo wa "Nguvu huvunjwa na pesa" umetumiwa kuonyesha nguvu za pesa katika jamii.
Shairi la "Mlima wa Kimombo" nalo limetumia methali kadhaa kuwa njia ya jadi ya kupinga kukumbatia utamaduni wa kigeni bila kuchuja. Misemo na methali kama "Mtoto mwenye njaa haonyeshwi titi," "Muwinda ndege huzunguka apajue mahali mtama ulipomalizwa na ndege," "Utokapo nje huwa kware," "Uzuri wa tunda la mtwetwe ndani limeoza," "Anayekohoa na kutema huwa anapunguza ugonjwa," "Mto unaotiririka haurudi nyuma," na kadbalika; ni raifano mizuri ya pamna misemo na methali vinavyotumiwa kuyajenga maudhui. Kwa mfano, katika methali ya "Mto unaotiririka haurudi nyuma" kuna fundisho la kutokukata tamaa katika harakati za kujikomboa; fundisho ambalo ndani yake pia lipo tumaini la ushindi.
Ishara ya Ngoma
Katika baadhi kubwa ya jamii za Afrika, ngoma hutumika kwa wito au kwa ajili ya vifijo na hoihoi za ushangiliaji.
Katika Malenga wa Bara, ngoma imetumika kwa makusudi hayo hayo. Katika shairi la "Kwenye Safari Barabarani", kwa mfano, washairi wanasema:
10. Najinsi tuendeavyo lengo lile,
Ndivyo jinsi ngoma zetu lelelele,
Ziongezavyo mipwito ya kelele
Kelele zizochangamana rajua.
Mipwito hii ya ngoma ni ishara ya ushindi ambao hauna budi kupatikana katika vita vya ukombozi wa watu wanyonge.
Shairi la "Sherehe" (uk.49) pia limetaja ngoma katika beti zake nyingi likieleza jinsi "ngoma mafungu mafungu" zitakavyochezwa katika sherehe hii (ambayo hata hivyo, hatuoni msingi wake). Ni sherehe, vicheko, vifijo na ushangiliaji wa jambo ambalo washairi hawatuonyeshi kinagaubaga kuwa ni jambo gani.
Mstari wa mwisho kabisa wa shairi la "Namna Tunavyoishi", unasema: "Kwa sababu haisiti, ngoma mpya ya dunia." Hii "ngoma mpya ya dunia," sawa na ile tuikutayo katika shairi la "Ngoma ya Radi", ni tangazo la maisha mapya; ni mbiu ya mgambo kuhusu maisha ya usawa, haki na upendo baina ya watu watakapojikomboa.
Taswira za Usambamba au Ulinganishi
Taswira ziitwazo za usambamba au za ulinganishi ni zile ambazo hutupa nyuso mbili za jambo katika kujenga maudhui fulani. Kwa mfano, katika riwaya ya Kasri ya Mwinyi Fuad, (TPH, 1974) taswira ya usambamba mapatikana katika maelezo ya rana na anasa za masikani ya mamwinyi yalinganishwapo na maelezo ya umaskim na unyonge wa masikani ya watu wa hali za chini kama vile nyumbani kwa Mzee Sharwani.
Kwa upande wa ushairi pia, taswira za usambamba zimetumiwa na washairi tofauti. Tutatoa mifano nuwili ya mashairi yaliyotumia taswira za namna hii katika Matenga wa Bara. Mashairi hayo ni ya "Sima na Mayai" na "Habari Mpya."
Katika shairi la "Sima na Mayai," maelezo ya maisha ya mkulima masikini (beti za 2, 4, 6, 8, 10, 12, 13, 14, 15, 16, 17) yameelezwa, sambamba na yale ya msomi mwenye nafasi nzuri kiuchumi (beti za 1, 3, 5, 7, 9 na 11). Usambamba huu unatusaidia katika kulinganisha maisha ya watu wa aina hizo mbili.
Kutokana na taswira hizi za mlinganisho sisi wasomaji tunaiona sima ya mtama upande nunoja, na upande wa pili tunaliona rundo la mayai si kwa maana ya moja kwa moja ya vyakula hivyo, bali kwa dhana iletwayo na mlinganishao wa taswira hizi mbili. Katika mlinganisho huu tunapata ufafanuzi wa ndani zaidi unaohusu masuala ya elimu, siasa, uchumi, utaroaduni na utabaka wa jamii.
Taswira za usambamba na za mlinganisho zinajitokeza pia katika shairi la "Habari Mpya". Humu tunalinganisha maneno ya Kasisi na ya "kijana mmoja pandikizi", na hatimaye Kasisi anapofariki, tunaupata ujumbe uliokusudiwa.
Majigambo
Matumizi ya majigambo si jambo geni katika ushairi wa Kiswahili. Tangu zamani yamekuwa yakitumika sana, hasa katika mashairi ya malumbano ambamo washairi walijitapa na kuringia ushairi wao kwa nia ya kuwadunisha washairi wengine walio "adui" zao katika mijadala mbalimbali.
Katika Malenga wa Bara mbinu hii ya majigambo haikutumiwa sana, na pale ilipotumiwa imeongeza nguvu za shairi linalohusika. Katika shairi la "Kauli ya Ununa" (uk.89) kwa mfano, washairi wameonyesha nguvu za kauli ya umma kwa majigambo yaliyojengwa ndani ya tamathali ya sitiari. Umma umeitwa "Nyundo" ambayo ina:
ulimi: ncha yenye kingo
Hukatisha nyemi, hubomoa nyongo

Ni mkoma wami ningiapo zogo.
Huu ni umma ulioshikamana kwa umoja kukataa ulwana.
Majigambo yamerudiwa katika shairi la "Soga" (uk.85) ambamo kwa njiaya ucheshi washairi wanapinga "Unyama" (bila hasa kutueleza ni unyama gani wanaouongelea) kwa kusema:
13. Jina langu Nyundo unanijua,
Kila nikidunda ninapasua...
14. Bali fuadini sitaki unyama!
Mtindo wa Tambo
Mtindo wa tambo hutumia mafumbo katika utoaji wa maudhui ya shairi. Tambo huwa sawa na kitendawili ambacho msomaji anatakiwa akifumbue. Katika malumbano washairi wengi walitumia mashairi ya tambu kuwafumbia washairi wenzao ili wakune vichwa kwanza kabla ya kuvumbua yale yaliyokusudiwa na waliyoaandika. Tumeona jinsi shairi ia "Vuteni Makasia" lilivyo tambo ambalo ndani yake mmejificha maana ya uhuru.
Shairi la "Usemi wa Nyoka" nalo ni la tambo. Limetumia ucheshi kwa kumtumia nyoka ambaye baada ya kujigamba mbele ya kadamnasi inambidi atoroke harakaharaka ili kujihami na ghadhabu za tembo. Katika fumbo hili liko fundisho kuwa kujitapa si tabia njema.
Shairi la "Asali na Nyuki" (uk. 83) nalo pia ni mfano mzuri wa aina ya tambo; na katika fumbo hili msomaji anaweza kutoa maana mbalimbali. Malhalani, asali huweza kuwa uhuru, mapenzi au jambo lolote lile analolitamani mtu hadi anajitolea kwa hali na mali ili alipate.
Mtindo wa Vina na Mizani
Katika diwani ya Malenga wa Bara, washairi hawakufungwa na mtindo wa aina moja wa ushairi. Humu imo mitindo mbalimbali, tangu ile ya kimapokeo yenye mpangilio mahsusi wa vina, mizani, na beti, hadi ile ya kisasa ambayo huamuliwa na kuainishwa na kile kiongelewacho. Kwa vile mtindo wa kimapokeo umezoeleka kwa baadhi kubwa ya wasomaji, hatutaushughulikia humu. Zaidi tutaangalia ile mitindo ambayo huenda ni migeni kwa wasomaji wengine japokuwa watakapoichunguza kwa undani wanaweza kuigundua hata katika nyimbo na ushairi wa makabila yao.
Katika shairi ia "Zuka" (uk. 7), washairi wameanza na ubeti ufuatao kanuni za kimapokeo kwa kutupa mistari yenye nuzani minane minane ambayo huishia na kina cha "ka". Ubeti wa pili wa shairi hili ni mchanganyiko wa mitindo ambamo ndani yake kina cha "ma" kimctawala. Wamefanya makusudi kabisa katika ukurasa uliotangulia kuandika katika mtindo wa mjazo uonekanao wa kinathari. Mtindo huu umetumiwa kwa sababu kubwa mbili: Kwanza, kuonyesha mabadiliko va msimuliaji kuwa sasa ni sauti ya watu na si ya msimuliaji wa nafsi ya kwanza; na pili, kuonyesha kuwa dhana ya mistari katika beti za shairi ni matokeo ya uandishi na kamwe isije kuchukulika kuwa kigezo cha sheria na kanuni za ushairi wa Kiswahili.
Baada ya hapo, washairi wamebadili tena mtindo na kutupa ubeti wenye kanuni sawa na ule wa kwanza. Kanuni hizi ni za mizani minane minane na kina cha "ja" kwani maneno ya ubeti huu yanatolewa na sauti nyingine. Hata katika ubeti unaofuatia yanatokea mabadiliko ya mtindo kwa sahabu hizo hizo. Hapa kuna kina cha "ji" ambacho kinatokea ndani kwa ndani badala ya kuwekwa katika sehemu mahsusi tu. ''Ubeti" wa mwisho, mfupi kuliko zote, ni wa hitimisho ambalo linabeba uzito wa aina yake:
Watu wanasikia,
Tangazo la zinduko jipya,
Mimi nimeshasiksa.
Ni wazi kuwa "tangazo hili" linaonyesha uzalendo uliopevuka zaidi ya ule wa kuipenda tu nchi tuukutao katika diwani ya kwanza ya washairi hawa ya Mashairi ya Kisasa.
Kuhusu vina, wakati mwingine washairi hawa wameviweka vina mwanzoni mwa baadhi ya mistari. Kwa mfano, katika shairi la "Jua la Dhahabu" ubeti wa tatu neno "Waka" limeleta vina na mapigo ya aina yake katika mianzo ya mistari kadhaa.
Washairi wanatumia sana mtindo wa marudiorudio ya maneno ili kusisitiza jambo, na wakati huohuo kuleta mapigo ya aina fulani. Kwa mfano katika mashairi ya "Siku Itafika" na "Siku Imefika" meneno ya vichwa hivyo yamerudiwarudiwa sana kusisitiza kwanza tumaini jema la wanyonge, na pili cherekochereko za ushindi. Vivyohivyo katika shairi la "Vilio vya Dhiki" jina la shairi limerudiwarudiwa kuonyesha wingi wa vilio hivyohivyo vinavyodai haki.
Katika shairi la "Sima na Mayai", japokuwa kuna kumdiwarudiwa kwa maneno "nikumbuke" na "kumbuka" ili kuwasisitizia vijana wasomi juu ya umuhimu wa kuikumbuka na kuitumikia jamii iliyowasomesha, mtindo hasa uliotumika ni ule wa ushairi huria wenye kulandana na msimuliaji (narrator) ambaye ni mkulima mzee na masikini.
Hii ni mifano tu ya baadhi ya mitindo waliyoitumia washairi hawa. Ni dhahiri kuwa iko mitindo mingi sana humu. Kwa mfano, japokuwa katika shairi la "Mlima wa Kimombo" mtindo wa vina na mizani wa kimapokeo unatumika, washairi wamechanganya pia mitindo mingine kufuatana na mambo tofautitofauti wanayoyashughulikia.
Mara nyingi wasimuliaji katika mashairi haya ni wa nafsi ya kwanza, "mimi", nafsi ambayo inafaulu kutufanya tuyaamini zaidi yale yasemwayo kuwa yanatokana na uzoefu wa kuyaishi maisha wayaelezayo.
Labda kwa kumalizia tungetahadharisha tu kuwa Kahigi na Mulikozi hawana vita wala uadui na ushain wa kimapokeo. Kwa hakika tukichunguza sana zaidi ya nusu ya mashairi yao katika Malenga wa Bara ni ya kimapokeo yenye kuzirigatia masuala ya vina na mizani. Jambo hili ameshindwa kuliona Jumanne Mayoka ambaye upinzani wake katika kitabu chake cha Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka (TPH, 1986) unaonyesha dhahiri kuwa hajakisoma kitabu cha Malenga wa Bara. Tena wakati mwingine katika kujaribu kuzingatia mno vipengele hivi vya vina na mizani baadhi ya mashairi ya Kahigi na Mulokozi yamekuwa na udhaifu. Kwa mfano katika shairi la "Kwa Shaaban Robert" ili kuleta mlingano wa kina cha "ni" kwenye beti za 3, 8, na 9, washairi wametumia maneno "uliyoyaandikeni", "uliyotu-achieni" na "tunakuoneni", ambayo husemwa kwa watu wengi na si kwa mtu mmoja kama walivyofanya hapa.
Udhaifu mwingine ni ule wa kawaida wa ngonjera za Mnyampala ambamo mhusika mmoja hubadilika ghafla katika msimamo wake. Katika "Ngonjera" (uk.43-49), ni vigumu kuamini mabadiliko ya mawazo ya Kijana anayeamka ghafla na kuwa mwanamapinduzi wakati ambapo muda mfupi sana uliopita alikuwa mbumbumbu hasa.
Hata hivyo, ni dhahiri kwamba Kahigi na Mulokozi wamefaulu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii-ya siasa, utamaduni na uchumi - katika mashairi yao kwa kutumia ufundi wao wa t'ani katika kuyatolea maudhui ya Malenga wo Bara.
Maswali
1. "Kahigi na Mulokozi wamefaulu kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii na pia katika ufundl wao wa kisanii kwenye Malenga wa Bara "Jadili.
2. "Kahigi na Mulokozi wanashauri katika baadhi kubwa ya mashairi yao kwamba watu washike marungu, mapanga, bunduki na risasi wauane bila sababu za kuridhisha." Jadili hoja hii na uthibitishe kwa mifano dhahiri.
3. Je, mawazo ya Kahigi na Mulokozi kuhusu Mungu, dini na maana ya maisha ni yapi katika Malenga wa Bara? Unayaonaje mawazo hayo?
4. Chagua dhamira mbili kati ya zifuatazo na ujadili zilivyojitokeza katika diwani ya Malenga wa Bara:
(a) Maanayauhuru
(b) Kumtetea mkulima
(c) Uzalendo
(d) Mapenzi.
5. Jadili kufaulu au kutokufaulu kwa fani ya mashairi ya Malenga wa Bara katika kuyashughulikia maudhui.
6. Chagua vipengele vitatu vya fani ya ushairi kati ya vifuatavyo na ujadili vilivyotumika katika Malenga wa Bara:
(a) Majigambo
(b) Misemo, methali na nahau
(c) Taswira ya safari
(d) Ishara
(e) Tamathali za semi.